Madiwani wa CCM waliopigana kuanza kuhojiwa

MADIWANI wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, wataanza kuhojiwa na vikao vya CCM ngazi ya wilaya kabla hawajachukuliwa hatua za kinidhamu.

Katibu wa CCM, Wilaya ya Kwimba, Abbass Mwajuki, aliiambia MTANZANIA kwa simu, kuwa madiwani hao wataanza kuhojiwa wakati wowote kuanzia sasa baada ya suala hilo kuondolewa polisi na kurejeshwa katika vikao vya chama.

Mwijuki alisema kuwa, madiwani hao watahojiwa na vikao vya Kamati ya Usalama na Maadili, kisha suala lao litapelekwa katika vikao vya juu zaidi kwa ajili ya kuchukua hatua za kinidhamu kwa kuwa madiwani walipigana katika ukumbi wa kikao cha Baraza la Madiwani.

“Suala la madiwani hao tayari limeshatoka polisi na halikupelekwa mahakamani bali limeletwa kwetu sisi kama chama kwa ajili ya kushughulika nalo.

“Kwa hiyo, kuanzia wiki ijayo, tutaanza kuwahoji madiwani hao kisha kutoa adhabu kutokana na vitendo walivyovifanya,” alisema Mwijuki.

Mwijuki alisema taratibu za chama chao ni kuwaita wahusika na kuwahoji na kama suala hilo ni kubwa zaidi, ngazi za mkoa na taifa zina jukumu la kutoa karipio kali na kuwavua wahusika uanachama hivyo kupoteza nafasi zao.

Katika suala hili, madiwani waliopigana ni Shija Malando wa Kata ya Hungumalwa na Tabu Mganga wa Kata ya Mhande.

Baada ya wanasiasa hao kupigana, walikamatwa na kushikiliwa katika Kituo cha Polisi, Wilaya ya Kwimba kwa mahojiano zaidi.

Baada ya kukamatwa, viongozi wa CCM waliwaomba polisi wasilifikishe suala hilo mahakamani, badala yake walijadili wao katika vikao kabla yakuchukua hatua dhidi ya wahusika.

Hata hivyo, baadhi ya madiwani wa CCM waliozungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotaja majina yao, walionyesha kutoridhishwa na hali hiyo, badala yake wakataka suala hilo lifikishwe mahakamani ili liwe fundisho kwa wanasiasa wengine.

chanzo : mtanzania
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment