Lwakatare Hoi

Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare
                                                                   *Chadema wahaha kumnasua bila mafanikio
                                                                   *Kova kuanika maadui waliomteka Kibanda

HALI ya afya ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare ni utata mtupu. Habari za kuaminika zilizopatikana jana mjini Dar es Salaam, zinasema afya ya Lwakatare imezidi kuzorota kutokana na ugonjwa wa kisukari unaomsumbua. Lwakatare alikamatwa Machi 13, mwaka huu kwa tuhuma za kupanga njama za kudhuru watu, ambapo anaonekana kwenye CD akipanga mikakati mbalimbali.

Hata hivyo, siku mbili baada ya kushikiliwa, Lwakatare alianza kulalamika kwa wakili wake, Nyaronyo Kicheere kuwa hajisikii vizuri kutokana na ugonjwa wa kisukari alionao, huku akishindwa kula chakula.

Kutokana na hali hiyo, jana Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa kwa mara nyingine alilijia juu Jeshi la Polisi, kwa kile alichodai linapanga njama za kutaka kumdhuru Lwakatare.
“Nasikitishwa na kitendo cha polisi, kuendelea kuwa na siri juu ya afya ya kiongozi wetu, haiwezekani jeshi la polisi lichezee afya ya mtu kiasi hiki… nasema umefika wakati sasa lijipange kwa jambo lolote litakalotokea kwa Lwakatare.

Alisema anashangazwa na kitendo cha polisi kushindwa kutoa ushirikiano na mawakili wa Lwakatare, pamoja na viongozi wa CHADEMA, jambo ambalo linaleta wasiwasi kuwa kuna mpango wa siri dhidi ya viongozi wa CHADEMA.

“Mwandishi unachotaka kujua juu ya Lwakatare ni kweli, lakini binafsi nashindwa nikueleze nini kwa sababu polisi hawataki kushirikiana na mawakili wa Lwakatare, wala sisi viongozi wa chama.

“Hapa nilipo sina taarifa yoyote kutoka kwa mawakili wa Lwakatare, najiuliza maswali mengi na kukosa majibu sijui polisi wanataka kitu gani, kitakachotokea watabeba lawama.

“Sijui polisi wana mpango gani na Lwakatare, kwani vitendo anavyofanyiwa haviendani na tuhuma zake, itakumbukwa siku moja baada ya kukamatwa, tulipeleka chakula polisi hawakutaka kukipokea, uliona wapi mtuhumiwa anazuiliwa kula chakula.

“Kama ambavyo hawatoi ushirikiano kwa vyombo vya habari, nasi hata simu zetu hawapokei. Kwa upande wa chama tunashindwa cha kuwaambia naombeni muwabane polisi wawaeleze kinachoendelea na walichopanga kesho (leo),” alisema.

Alipoulizwa kama chama kina mpango gani kutokana na afya ya Lwakatare kuendelea kuzorota rumande, alisema kwa kuwa suala hilo lipo kwenye vyombo vya sheria, wanawaachia mawakili wao.

Hivi karibuni Wakili wa Lwakatare, Kicheere alinukuliwa na vyombo vya habari akidai mteja wake ameshindwa kula chakula kutokana na matatizo ya ugonjwa wa kisukari.

Alisema mteja wake anatembea kwa kujivuta, kitendo kinachomtia hofu kutokana na hali halisi aliyomwona nayo na kuongeza kwamba, anahangaika sana kuhakikisha anapata dhamana lakini haoni matunda.

“Mteja wangu ni mgonjwa wa kisukari, kwa kawaida hutakiwa kula chakula na kunywa maji mengi, lakini nimehangaika sana, leo (jana) nilikuwa na matumaini kwamba, atapelekwa mahakamani ambapo nilijipanga kwa kuandaa watu makini wenye hati za nyumba nikiwa na imani kwamba angepata dhamana, lakini wamemrudisha mahabusu,” alisema Kicheere.

MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova kuzungumzia hilo simu yake iliita bila kupokelewa.

Alipotafutwa kwa mara nyingine kwa nyakati tofauti, simu yake iliita na kuzimwa, hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu.

KOVA KUANIKA UKWELI

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo linatarajia kuanika majina ya watu wanaodaiwa kumteka na kumtesa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda.

Habari zinasema Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova atakutana na waandishi wa habari kueleza ukweli au kutaja majina ya watu ambao wamekuwa wakisubiriwa kwa shauku na jamii. Hadi jana walikuwa wakimshikilia mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Joseph Ludovick, akihusishwa na matukio mengi yanayohusiana na tukio la kutekwa Kibanda.chanzo : mtanzania
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment