Watu wenye ulemavu nchini wamekuwa wakikabiliwa na
changamoto mbalimbali katika maisha yao ya kila siku, kama ilivyo kwa
wategemezi wao.
Christina Mauma, mwenye umri wa miaka 46, ni miongoni
mwa watu wenye ulemavu wanaokabiliwa na changamoto hizo, ambazo zinatishia
mustakbali wa elimu ya mwanae mwenye umri wa miaka 8.
Christina, mkazi wa eneo la Kiara Musoma alizaliwa akiwa
na matatizo ya macho na kutokana na uduni wa hali ya kipato cha mama yake,
hakuweza kupata matibabu ya kisasa kwenye hospitali yoyote na hivyo kuamua
kutumia dawa za kienyeji.
Dawa hizo hazikumsaidia, jambo ambalo lilimfanya mama
yake, Bi. Nezia Siti, kukubaliana na uhalisia kuwa binti yake atakuwa kipofu.
Hata hivyo, Christina alichukua mafunzo ya ufumaji katika
chuo cha Singida College mkoani Singida, lakini kwa bahati mbaya mambo hayakuwa
mazuri kwa kuwa wateja wengi wanapendelea bidhaa za kisasa.
Baada ya kumaliza mafunzo yake, alirejea Musoma na
kuanzisha biashara ya ufumaji wa vitu mbalimbali kama vile soksi za watoto,
kofia na sweta. Lakini biashara haikuwa nzuri kwa kuwa watu wanapendelea bidhaa
za viwandani kuliko zile zinazotengenezwa kienyeji.
Aliamua kufunga biashara yake na kukaa nyumbani, hali
iliyotishia ustawi wa mtoto wake Baraka Ezron mwenye umri wa miaka 8, ambaye
anasoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Kiara mjini Musoma.
0 comments:
Post a Comment