VITUKO: MTAA WA UNAOTUMIA NOTI YA PESA TOFAUTI NDANI YA NCHI MOJA

Bangla-pesa
Wakazi wa mtaa wa Bangladesh, Changamwe wakitumia Bangla-pesa kununua dagaa almaarufu omena.





WAKAZI wa mtaa wa mabanda wa Bangladesh, eneo la Changamwe, Mombasa, wana pesa tofauti na Wakenya wengine, ambazo wanatumia kulipia bidhaa na huduma.

Pesa hizo, ambazo wanaziita Bangla-pesa, zimekuwa zikitumika kwa muda wa wiki mbili sasa. Unapotembea mtaa huo, ni vigumu kutambua kwamba hizo sio pesa rasmi za nchi. Noti hizo, ambazo za 5,10,20 na 50 zimewekwa muhuri na nembo rasmi kuthibitisha uhalali wake kwa watumiaji.


Waanzishishi wa mpango huo wanasema unanuiwa kusaidia familia zinazoishi katika mtaa huo ambao wanadai kuwa pesa za hazipatikani kwa urahidi.
Afisa mkuu wa mradi huo, Bw Alfred Sigo, anasema dhana ya kubuni pesa hizo ilitokana na Will Ruddick, raia wa Amerika, ambaye anasema lengo lake si kupuuza pesa za kitaifa bali kuinua hali ya maisha na kukuza uchumi wa wakazi wa Bangladesh.

Noti hizi huchapishwa na kampuni ya Punchlines Printing Security, jijini Nairobi na kusafirishwa hadi Mombasa chini ya ulinzi mkali. “Awali, tulitaka kuipatia kampuni ya De la Rue kandarasi ya kutuchapishia pesa hizi lakini ikawa ghali sana ndiposa tukapatia Punchlines,” anasema Bw Sigo.

Michoro katika noti hizo inahusu maisha ya wakazi wa Bangladesh. Baadhi ya noti hizo zina michoro ya kuashiria shughuli za wakazi za kujipatia riziki kama vile wakulima shambani, kina mama wakishona nguo na wengine wakiunda vikapu. “Hivi sasa tunaendelea kuunda katiba itakayodhibiti matumizi ya pesa hizi na  katika mkutano mkuu wetu ujao tutawasilisha stakabadhi kwa Serikali ili kusajili mradi huu kuwa wa kijami,” Bw Ruddick akaambia Taifa Leo kwa simu.

Alisema chifu wa eneo hilo ametishia kuwachukulia hatua za kisheria kwa sababu hawajasalisha mradi huo. “Amekuwa akisema tunaendesha biashara kwa kutumia pesa ambazo si rasmi,” akasema Bw Sigo.

Bw Ruddick alisema kuzinduliwa kwa pesa hizo kumeimarisha biashara katika eneo hilo kwa asilimia 22. “Miradi ya aina hii imefaulu katika mataifa mengine, kama vile Uswisi na tunakusudia kuueneza katika kaunti nzima ya Mombasa,” akasema.

Kila mwanachama hupewa Bangla-pesa 400 ambapo anatarajiwa kurudisha Bangla-pesa 200 na kutumia zilizobaki kununua bidhaa. Kabla ya kupewa pesa hizo, mtu anahitajika kuwa na wadhamni wanne ambao watamsaidia kulipa akishindwa. Mwanachama na wadhamini wake wanaoshindwa kulipa wanaondolewa katika mradi huo.



PICHA YA BANGLA-PESA






BANGLA-PESA 400

Ili kudhibiti usambazaji wa Bangla-pesa, kila mwanachama anakubaliwa kutumia Bangla-pesa 400 pekee kwa siku. “Thamani ya Bangla-pesa si sawa na ile ya shilingi ya Kenya bali imewekwa chini ili iweze kukubalika na wanachama wetu walio na mapato ya chini,” anasema Bw Sigo.

Mradi huo umefadhiliwa na shirika la kijamii kwa jina Koru, linaloongozwa na Bw Ruddick. “Kutokana na mradi huu, sasa hatutegemei msaada wa Serikali, tunajiendeleza sisi wenyewe,” akasema mmoja wa wanachama.

Mtaa wa Bangladesh una watu zaidi 22,000 na umegawanywa katika vijiji saba vinavyotumia Bangla-pesa.

Bw Sigo alisema hatua hii inakusudia pia kubadilisha dhana kuwa Bangladesh ni eneo lisilo salama na kuwa wenyeji hujihusisha tu na uhalifu. “Kushirikisha wakazi katika mradi huu kutaondoa kasumba kuwa ni mtaa uliosakamwa na wahalifu tu, tunataka kuona watu wakijiendeleza kibiashara na kimaisha,” akasema.

“Kufikia mwisho wa mwaka huu tunalenga kuwezesha wanachama kutuma na kupokea Bangla-pesa kwa simu,” akasema Bw Sigo.

Wafanyabiasha wote huweka mabango nje ya biashara zao kuonyesha kuwa wanakubali Bangla-pesa kulipia bidhaa na huduma.



Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment