Barack Obama: Kwa nini anakuja Tanzania, Afrika?

Barack Obama
Na Simon Mwalwimle
 
KATI ya taarifa kubwa za kimataifa kuhusu Bara la Afrika, zilizotolewa wiki iliyopita ni ziara ya pili ya Rais Baraka Hussein Obama wa Marekani katika nchi za Tanzania, Rwanda, Afrika Kusini na labda Nigeria ikitegemea hali ya usalama nchini humo.
Ziara hii, inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwezi ujao wa Juni, ni ya pili kwa Afrika kwa Obama akiwa Rais ikitanguliwa na ile aliyoifanya Julai mwaka 2009, Ghana.
Obama mtoto, ambaye marehemu baba yake, naye pia anaitwa Baraka Hussein Obama (18 Juni 1936 - 24 Novemba1982) ni Mwafrika mzaliwa wa Kenya akitokea eneo la Rachuonyo kandokando ya Ziwa Victoria, alikulia kijiji cha Nyang’oma Kogelo eneo la Nyanza nchini Kenya.
Hapa Tanzania wakati tukisubiri ziara ya kiongozi wa taifa kubwa kiuchumi duniani, kuna maswali kadhaa tunapaswa kujiuliza. Kwa nini anakuja? Au, anakuja kufanya nini? Kwa nini sasa?
Labda, kabla ya majibu ya maswali haya, tukumbushane kuwa marais wa Marekani wa karibuni, wote wametembelea Tanzania. Bill Clinton amekuja mara kadhaa ikiwa ni pamoja na mwaka 1998 wakati Rais George Bush alitutembelea mwaka 2008.
Ni ishara njema kutembelewa na wageni hususan pale wanapokutembelea ukiwa salama, hakuna vita wala ugomvi. Wanafika kukusalimu, kubadilishana mawazo na kukupa ushauri wa hapa na pale.
Kwa msingi huu, ugeni huu si kama ule wa wanajeshi wa Tanzania waliokwenda Mashariki wa Congo hivi karibuni kusimamia amani. Lakini, nini hasa kinamleta Obama (51) Tanzania na Afrika?
Hali ya usalama Afrika

Jambo la kwanza tunalopaswa kukubaliana ni kwamba maslahi ya kiusalama, kiuchumi na kijamii yametapakaa duniani kote. Wamarekani na kampuni zao wapo kila kona ya dunia wakifanyabiashara na shughuli mbalimbali za kijamii na hivyo wanahitaji ulinzi.
Bila shaka, Afrika pia wamo na tunawaona na ndiyo maana kuna chombo kiitwacho USARAF (United States Africa Army) na AFRICOM (United States Africa Command). Kimsingi, kwa mujibu wa Marekani, lengo la vyombo hivi, pamoja na kusimamia maslahi ya Marekani barani Afrika, pia ni kusisimua na kuhamasisha mabadiliko chanya katika Bara la Afrika kwa kuzima vikundi vyenye misimamo mikali (violent extremist organisations) na hivyo kutengeneza mazingira salama kwa biashara na ukuaji wa demokrasia.
Bila shaka, katika hili nchi zote zilizotajwa kuwa Obama atazitembelea zina nafasi kubwa ya kuyasimamia haya. Tanzania inafahamika, tangu miaka ya uhuru na hadi sasa, kama kinara wa masuala ya kuimarisha usalama barani Afrika. Uthibitisho wa karibuni kabisa ni jitihada za kurudisha amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Madagascar na hata Zimbabwe.
Rwanda, kwa upande wake inatajwa kama kiungo muhimu cha amani katika eneo tete la Mashariki ya DRC. Inawezekana pia ziara hii ya Obama ni kuzitia moyo Tanzania na Afrika Kusini ambazo zimewatoa askari na maofisa wake kwenda DRC kuimarisha amani. Hii pia inaweza kuikumbusha Rwanda kujitahidi kuondoa hisia katika anga za kimataifa kuwa nchi hiyo inahusika na vita hiyo isiyoisha Mashariki mwa DRC na kusini mwa Rwanda.
Lakini Rwanda ina nafasi nyingine zaidi. Pamoja na kutokuwa na bandari na historia ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, Rwanda ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7 kwa mujibu wa Benki Kuu ya nchi hiyo, kasi kubwa kuliko ile ya asilimia 4.8 ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa mujibu wa tathmini ya Benki ya Dunia (Africa’s Pulse, 2012).
Kwa sababu hii, Rwanda imekuwa ikipigiwa mfano na wakubwa ikiwemo Marekani si katika uchumi tu, bali hata katika kusimamia masuala mtambuka ya kimataifa kama usawa wa kijinsia. Na ni ukweli ulio wazi kwamba, nchi hizi tatu (Tanzania, Rwanda na Afrika Kusini) ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo muhimu vya uamuzi, zote zimepita asilimia 30 iliyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Kwa hiyo, itakuwa sahihi kusema kuwa kiongozi yeyote mkubwa duniani, kama Obama, angependa kuitembelea Rwanda na hizi nyingine ili kuwaamsha wengine kuiiga.
Nigeria na Afrika Kusini ni mataifa makubwa kiuchumi kwa Afrika. Kwa taifa kubwa kama Marekani, hizi ni nchi ambazo inabidi ikae nazo meza moja na kuzungumza namna bora ya kufanya biashara hususan wakati huu ambao taifa jingine kubwa kama China linawekeza kwa kasi Afrika. Na hili linaweza kutupa hoja ya nyingine ya ziara ya Rais wa China Africa, mapema mwaka huu.

Kufuta nyayo za Rais wa China

Itakumbukwa kuwa ni Rais wa China Xi Jinping, aliyechaguliwa Machi 14, mwaka huu alifanya ziara ya siku sita Afrika kuanzia Machi 24 mwaka huu.
Ziara hii ilimwezesha kutembelea nchi za Tanzania, DRC na Afrika Kusini. Kati ya hizi, tunaambiwa kuwa Obama atazuru Tanzania na Afrika Kusini.
Katika ziara hii, Jinping alitia saini mikataba mikubwa na nchi hizi ikiwemo aliyosaini na Tanzania iliyolenga kuimarisha miundombinu kama ujenzi wa bandari kubwa na ya kisasa Bagamoyo na uimarishaji wa reli.
Kwa ufupi, akiwa Tanzania alisaini mikataba 17 ukiwamo ule wa miaka mitatu wa ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi wenye thamani Sh trilioni 1.8 (Dola za Marekani milioni 800).
Itakumbukwa pia kuwa China ni taifa la pili kwa ukubwa kiuchumi duniani, nyuma ya Marekani. Bila shaka, hata ningekuwa mimi, nisingekaa kimya nikikodolea macho hali hii bila nami kuchukua hatua.
Nadhani, Obama atapenda pia kufuta zile nyayo za Jinping ambazo baadhi ya wadau wanaamini zimekwishajikita na itabidi kutumia nguvu za ziada kuzifuta kwa sababu zina historia ndefu tangu enzi za Mwalimu Nyerere. Kwa vyovyote vile, nchi za kiafrika, ikiwemo Tanzania, tuwaache wakitukimbilia ili ule msemo, Mgeni Njoo, Mwenyeji Apone, utimie.

Kenya na ICC

Tunafamu kuwa viongozi wakuu wa majirani zetu Kenya, Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Rutto wanakabiliwa na tuhuma za kupanga na kuchochea vurugu za baada ya uchaguzi nchini mwao mwaka 2008.
Viongozi hawa wawili, pamoja na tuhuma hizo, walipewa ridhaa na kuongoza Kenya na wananchi kupitia uchaguzi wa kidemokrasia tena chini ya Katiba Mpya inayopigiwa mfano na wadau wengi ndani na nje ya Afrika.
Hali hii, inaelekea haijawahi kuwafurahisha wakubwa hata kidogo. Kuna baadhi yao walitishia, kabla ya uchaguzi, kuwa wangesitisha ushirikiano na Kenya iwapo wawili hao wangechaguliwa kuiongoza nchi hiyo yenye uchumi mkubwa katika Afrika Mashariki.
Kwamba Kenya haimo katika ratiba ya ziara ya Obama kwa Afrika halipaswi kuwa jambo geni kwa wanaofuatilia masuala ya Marekani na Kenya. Obama, pamoja na kuwa baba yake mzazi alitokea nchini humo, hajawahi kuitembelea nchi hiyo akiwa Rais ukiondoa ile ziara yake ya mwaka 2006 akijiandaa kugombea urais nchini Marekani.
Kama anavyowahi kusema Kwaku Osei, mchambuzi wa masuala ya siasa na mzaliwa wa Ghana, suala la Kenya na ICC ni kati ya mambo yanayoiumiza kichwa Marekani na ICC, Mahakama ambayo inalalamikiwa na baadhi ya waafrika kuwa inaliandama bara hili.
Kwa hiyo, pamoja na sababu nyingine nyingi za Obama kutarajiwa kutembelea nchi mbili (Tanzania na Rwanda) kati tano zinaunda Jumuiya ya Afrika Mashariki (Kenya ikiwemo), tunaweza kutaja sababu nyingine ni kuwatia wivu ndugu zetu wa Kenya. Ni kama kuwaambia, ‘pamoja na kuwa nina damu ya Kenya, kwa sasa sitafika huko hadi haya mambo ya ICC yaishe.’
Lakini wakati Obama akisema haya, tunaweza kusema angependa kujenga uhusiano mzuri na majirani wa Kenya hiyo hiyo ambao inaelekea wanaiunga mkono Kenya katika jitihada zake za kuanza ukurasa mpya wa kuijenga nchi yao na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hili linathibitishwa na ushiriki wa viongozi wa nchi wanachama katika sherehe za kuwaapisha Kenyatta na Rutto pale katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi siku ile ya Aprili 9, mwaka huu.

Mchakato wa Katiba Tanzania

Ukweli kwamba Watanzania wapo katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya itakayotoa mustakabali wa mambo kadhaa ya nchi yao, linaweza kumvutia kiongozi mkubwa kama yeye.
Kwa namna mchakato unavyoendelea, ni imani ya wengi kuwa mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya utakwisha salama. Labda kinachoweza kumvutia Obama ni  hatma ya Muungano, hususan baada ya maoni yanayokinzana kutoka kwa baadhi ya wadau – mengine yakiashiria uimarishwe na mengine, kwa kweli yakiashiria kuuvunja nguvu au kuubomoa kabisa.
Ukweli ni kuwa maoni yanayoashiria kuubomoa hayakubaliki na wengi wetu kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kiusalama katika Pwani ya Bahari ya Hindi. Na bila shaka hili halikubaliki na hata marafiki zetu na wadau wengine ikiwemo Marekani.
Kwa kuwa taarifa zinaeleza anaweza kuzuru nchini mwishoni mwa Juni, muda ambao tunaamini rasimu ya Katiba yetu (mpya) itakuwa imetolewa na Tume ya Jaji warioba, basi tutumaini kuwa wakati huo suala hili la Muungano litakuwa limefikia pazuri. Tusubiri.

Utamaduni wa kupokezana vijiti

 
Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na mgeni wake, Barack Obama wote wapo katika vipindi vya pili na vya mwisho vya uongozi katika nchi zao.
Kwa kuzingatia mazingira hayo, unaweza kujiuliza swali je, nini watafanya baada ya kustaafu? Inawezekana, nalo hili wanaweza kuulizana (JK na Obama) wakikutana hapo mwishoni mwa mwezi ujao.
Lakini, katika hili kuna kubwa zaidi. Umuhimu wa kupeana vijiti katika uongozi. Nchi zote anazotarajia kutembelea Obama, isipokuwa Rwanda, zimekuwa na utaratibu (uliokwishawahi kutumika kwa miongo kadhaa) wa kikatiba wa ukomo wa madaraka ya urais na umekuwa ukiheshimiwa.
Tangu enzi za Mwalimu Nyerere Tanzania tumeheshimiwa kukabidhiana madaraka kwa amani. Mwalimu alimkabidhi Mzee Ali Hassan Mwinyi mwaka 1985 naye kukabidhi kwa Benjamin Mkapa (1995) na baadae kwa JK mwaka 2005.
Hili pia linatokea Marekani, Afrika Kusini na Nigeria. Unaweza kusema, Obama atataka kuwaambia wengine, ikiwezekana majirani zetu, kuwa hili linawezekana na wafanye hivyo.
Kwa kumalizia, kwa vyovyote vile, kama ilivyokuwa kwa ziara ya Rais wa China, ni matarajio ya wengi kuwa ziara hii italeta tija kwa pande zote mbili.

CHANZO : RAIA MWEMA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment