UTURUKI YAJITOSA MGOGORO WA GAZA


Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akizungumza katika Chuo Kikuu cha Cairo Novemba 17, 2012
WAZIRI Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa utawala wa Israeli utalipa gharama -- sasa au baadaye -- kwa kuuwa watoto wasiokuwa na hatia katika wimbi la mashambulizi yanayoendelea dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Cairo nchini Misri jana Jumamosi, Erdogan alisema kuwa kwa mara nyingine Israeli imetekeleza kila aina ya vitendo vilivyo kinyume na ubinaadamu na kuligeuza eneo lote kuwa bwawa la damu, akaongeza kuwa Uturuki inalaani vikali vitendo hivyo. Hayo yaliripotiwa na shirika la habari la Uturuki, Anatolia. 

Vile vile aliapa kuwaunga mkono Wapalestina na kuitaka Israeli ikomeshe mashambulizi yake. 


Wimbi jipya kabisa la mashambulizi ya Israeli kwenye Ukanda wa Gaza limeua watu 46 kwa uchache tangu Novemba 14. Ahmed al-Ja'abari, kiongozi maarufu na mwenye ushawishi wa tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi za Ezzedeen al-Qassam, aliuawa katika mashambulizi ya Israeli yaliyolilenga gari lake siku ya Jumatano.

Siku ya Ijumaa, Ahmed Abu Jalal, kamanda wa ardhini wa Brigedi za Ezzedeen al-Qassam, aliuawa pia katika mashambulizi ya ndege za Israeli dhidi ya wilaya ya Maghazi katikati mwa Gaza.

Siku ya Jumamosi, ndege za Israeli ziliyashambulia majengo ya serikali ya Hamas, baada ya baraza la mawaziri la Israeli kuidhinisha kuwa askari 75,000 waliostaafu waitwe ili kujiandaa na uvamizi wa ardhi. 

Mara kwa mara jeshi la Israeli limekuwa likiendesha mashambulizi ya anga dhidi ya Ukanda wa Gaza, kwa madai kuwa vitendo hivyo vinafanywa kwa malengo ya kujilinda. Lakini hujuma hizo zimekuwa zikikiuka sheria na taratibu za kimataifa, kuwaua na kuwajeruhi raia.

Gaza imekuwa katika mzingiro wa Israeli tangu mwaka 2007, hali ambayo imesababisha kushuka kwa viwango vya maisha, ukosefu mkubwa wa ajira na umaskini uliokithiri.


 
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment