GAZA: WAIRAN 20,000 WAJIANDIKISHA KWENDA KUPAMBANA NA ISRAELI
NA KABUGA KANYEGERI
SIku ya Jumatatu, watu wapatao 20,000 kutoka miji mbalimbali ya Iran walianza kuandikisha majina yao katika orordha ya kujitolea kupigana na Israel huku maelfu ya watu wengine wakitarajiwa kujiunga leo.
Kiasi cha wanafunzi 7,000 katika mji wa kati wa Iran wa Isfahan wamejitolea kwenda kuungana na Wapalestina kupambana na Israeli huku wanafunzi wengine wengi wakijiasajili katika mji wa Tehran.
"Katika siku ya kwanza ya kujiandikisha kupambana na utawala wa Kizayuni na kuwasaidia Wapalestina, wanafunzi 7,000 kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya mji wa Isfahan wametangaza utayari wao," Mohammad Zarifi, mwanachama wa Jumuiya wa Wanafunzi wa Kiiran aliiambia FNA.
Siku hiyo hiyo, kundi jengine la wanafunzi wa Kiiran, Wanafunzi wanaojitolea (Basij) kutoka vyuo vikuu vya Tehran, walitangaza kujiandikisha kwenda kupambana na Israeli.
Usajili huo umekuja siku moja baada ya kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei kutoa fat'wa ya kidini akisema kuwa yeyote atakayekufa katika kupambana na Israeli na kwa kuitetea Gaza atakuwa amekufa kishahidi.
Fat'wa hiyo ya kidini ya Ayatollah Khamenei haikuchukuliwa kama ni uamuzi wa serikali na haikuiwajibisha serikali kufanya mashambulizi dhidi ya Israeli.
"Katika kuitikia wito wa Kiongozi Mkuu wa Jihad (vita vitukufu), wanafunzi wa Basij kutoka vyuo vikuu vyote vya Iran wamejiandikisha na uandikishaji huo utaendelea kesho," alisema Alireza Zahedi, mwanachama wa Chama cha Wanafunzi wanaojitolea kutoka Vyuo vikuu vya Tehran, bila kueleza ni wanafunzi wangapi ambao wameshajisajili.
"Muda mfupi ujao, wanafunzi waliojiandikisha watafanya mkutano ili kutangaza mwitikio wao kwa Kiongozi Muadhamu kwenda kupigana katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu," aliongeza.
Katika kadhia hiyo hiyo, siku ya Jumatatu kundi la wanazuoni wenye ushawishi mkubwa wa kidini nchini Iran wamezindua mpango wa usajili kwenye mtandao kwa wale wanaotaka kujitolea kwenda kupambana na Israeli katika kujibu mashambulizi ya anga yanayofanywa dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Siku ya Jumatatu, kiasi cha watu 3,550 walijiandikisha kwenye mtandao huo wa Jumuiya ya wanazuoni hao wa kidini. Kampeni hiyo ya mtandaoni inawapa wale wanaotaka kujitolea njia tatu za namna wanavyoweza kupambana na Israeli: kijeshi, kifedha na propaganda.
Kundi hilo, ambalo lina nguvu na ushawishi mkubwa nchini Iran, halikutoa maelezo zaidi kuhusu programu hiyo yanayojumuisha jinsi watu hao wanavyoweza kuwasiliana nao au utekelezaji wa programu hiyo.
Takwimu zinaonesha kuwa watu wanaokadiriwa kufikia 20,000 wameshaandikisha majina yao katika miji mbalimbali nchi nzima.
Jumamosi asubuhi, Israel ilianzisha mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuuwa watu kadhaa na kujeruhi wengine wapatao 1750.
Mashambuliz hayo yamesababisha maandamano katika miji mbalimbali ya Iran na nchi nyingine ulimwenguni.
Maelfu ya Wairan, wakiwemo wanafunzi wa chuo kikuu, walifanya maandamano siku ya Jumatatu asubuhi kulaani mashambulizi ya Israeli katika Ukanda wa Gaza huku wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa nara na kauli za kuilaani Marekani na Israeli.
Baadhi ya mabango yalisomeka: "Mauti kwa Israeli," "Mauti kwa Marekani" na "Waislamu unganeni."
Israeli ilisema kuwa mashambulizi yake ya anga katika Ukanda wa Gaza ni "vita vya juma" dhidi ya Hamas na Naibu Waziri Mkuu Haim Ramon siku ya Jumatatu alisema , "Lengo la Operesheni hii ni kuiangusha Hamas."
Katika kujibu mashambulizi ya Israeli, wapiganaji wa Kipalestina walirusha makombora 80 kusini mwa Israeli yakawaua watu watatu na kuwajeruhi zaidi ya 35, baadhi yao vibaya kabisa. .
Tel Aviv imewaita askari 6,500 waliostaafu na kutumia vifaru katika mpaka wake na Gaza katika kujiandaa na vita vya chini dhidi ya ukanda wa pwani wenye Wapalestina milioni 1.5.
Vile vile, Siku ya Jumatatu, Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran, ilituma meli iliyobeba tani 2,000 za chakula kwenda kwa Wapalestina wanaoishi Gaza kupitia Misri. Ndege ya kijeshi ya Iran pia ilitua katika uwanja wa kimataifa wa Cairo ikiwa imebeba tani 24 za chakula na madawa kwa ajili ya Gaza.
Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu, Masoud Khatami, alisema meli nyingine tatu zinasubiri kupakia misaada ya kibinaadamu, na hospitali za Iran ziko tayari kuwapokea majeruhi kutoka Gaza.

0 comments:
Post a Comment