WAPALESTINA WATAKA TAIFA HURU LICHA YA TISHIO LA KURA YA VETO

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (picha ya maktaba)



Mamlaka ya Palestina imesema kuwa itaendelea na juhudi zake katika Umoja wa Mataifa za kutaka kutambuliwa rasmi kama taifa licha ya juhudi za pamoja za Marekani na Israel kukwamisha jaribio hilo.

Wapalestina watawasilisha azimio hilo leo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huku kukiwa na taarifa kuwa Washington na Tel Aviv zinatengeneza upinzani wa pamoja dhidi ya hatua hiyo, ambapo Marekani imekuwa ikitumia kura ya turufu kuzuia azimio lolote lisiloupendelea utawala wa Israel.

Hata hivyo, maafisa wa Kipalestina wanaonekana kutojali, wakisema kuwa watawasilisha azimio hilo ambalo linataka kuwekwe muda wa mwisho wa miaka miwili kwa Israeli kuondoa majeshi yake katika ardhi za Palestina inazozikalia kwa mabavu.

“Tutawasilisha muswada wetu kesho mbele ya Baraza la Usalama”, alisema mshauri wa Rais wa Palesina Mahmud Abbas hapo jana.

Aidha, Mwakilishi mkuu wa Palestina kwenye mazungumzo ya amani Saeb Erakat alitoa maelezo kama hayo wakati wa mazungumzo baina yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, John Kerry, mjini London, ambapo mwanadiplomasia huyo wa Marekani alionya kuwa serikali yake itazuia azimio lolote linalodai uhuru wa Palestina.

Kerry ameripotiwa kufanya mazungumzo kwa siku tatu na baadhi ya nchi za Ulaya katika jaribio la kuizima hoja hiyo.


Wakati huo huo Erakat alionya kuwa hatua ya Marekani kutumia kura ya veto itawafanya Wapalestina kuomba uanachama wa taasisi kadhaa za kimataifa ikiwemo Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), ambapo watakuwa na uwezo wa kuushtaki utawala wa Israeli kwa uhalifu na jinai za kivita.

Marekani pia inapinga juhudi ya Palestina kupata uanachama wa Mahakama ya ICC.

Kwa miezi kadhaa sasa, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Palestina imekuwa ikitaka kutolewa kwa azimio litakaloamua mipaka ya taifa la Palestina ya baadaye kwa mujibu wa mipaka ya mwaka 1967.

Mwaka 1967, Israel iliyakalia maeneo ya Ukingo wa Magharibi, Jerusalem Mashariki (al-Quds) na Ukanda wa Gaza lakini ikaondoka Gaza na kisha kuizingira  mwaka 2005.


Wapalestina wanataka kuundwa kwa taifa lao huru kwenye maeneo ya Ukingo wa Magharibi, Jerusalem Mashariki ya al-Quds na Ukanda wa Gaza.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment