| Waziri mkuu mpya wa Somalia Omar Abdirashid Ali Sharmarke akizungumza kufuatia uteuzi wake mjini Mogadishu, Somalia, Desemba 17, 2014. |
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amemteau balozi wa
nchi hiyo nchini Marekani kuwa waziri mkuu kufuatia kuondolewa kwa aliyekuwa
waziri mkuu mapema mwezi huu.
Akiwa katika viwanja vya Ikulu mjini Mogadishu leo
mchana, Rais Mohamud alimteua mwanasiasa mzito mwenye umri wa miaka 54, Omar
Abdirashid Ali Sharmarke kuchukua wadhifa huo.
"Nina furaha kumteua Omar Abdirashid Ali kuwa
waziri mkuu mpya wa nchi yetu. Ninatarajia kuwa atatekeleza majukumu yake,”
alisema rais huyo.
Rais Mohamud aliongeza kuwa Somalia iko njia panda na
inahitaji waziri mkuu mpya atakayeweka mipango makini kwa ajili ya mustakbali
wa kisiasa wa nchi hiyo.
Kwa upande wake Sharmarke alisema kuwa ataendeleza
juhudi za kuleta uthabiti na kuipeleka nchi kwenye uchaguzi ulio huru.
Sharmarke anachukua nafasi ya Abdiweli Sheikh Ahmed
Mohamed, ambaye bunge lilipiga kura kumuondoa siku 11 zilizopita kutokana na
mzozo mkubwa uliokuwepo kati yake na Rais wa nchi hiyo kuhusu mabadiliko ya
baraza la mawaziri na kuondolewa kwa mkuu wa upelelezi wa nchi hiyo.
Umoja wa Mataifa, Marekani na Muungano wa Ulaya zilionesha
wasiwasi kuhusu mgogoro uliokuwa ukiendelea katika Ikulu ya Somalia.
Sharmarke aliwahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo katika
serikali ya mpito iliyokuwa ikiungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kati ya
mwaka 2009 na 2010. Alijiuzulu baada ya kushindwa kuelewana na Rais wa wakati
huo Sheikh Sharif Sheikh Ahmed.
Sharmarke anakabiliwa na changamoto kubwa za kupambana
na ufisadi, kulishinda kundi la al-Shabab na kuijenga upya Somalia
iliyoharibiwa na vita.
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Nicholas
Kay amesema kuwa nchi hiyo ina mlima mkubwa wa kupanda ili kupitia katiba na
kufanya kura ya maoni itakayofuatiwa na uchaguzi mwaka 2016.
0 comments:
Post a Comment