Rais mteule wa Misri Abdulfattah al-Sisi |
Mkuu wa zamani wa jeshi la Misri, Abdul Fattah al-Sisi anaapishwa
leo Juni 8, kuwa rais mpya wa Misri.
Shirika la habari la serikali ya nchi hiyo, MENA,
limesema kuwa al-Sisi ataapishwa katika viwanja vya Mahakama Kuu ya Katiba.
Kwa mujibu wa taarifa huyo, rais wa mpito Adly Mansour, Waziri
Mkuu Ibrahim Mahlab na baraza lake, Mkuu wa chuo Kikuu cha al-Azhar, Papa wa
Kanisa la Wakopti Tawadros II, wanasiasa na watu wengine mashuhuri watahudhuria
sherehe hiyo.
Shughuli hiyo inafanyika wiki moja baada ya uchaguzi
uliofanyika Mei 28 na ambao ulichukua siku tatu mfululizo.
Katika matokeo yaliyotangazwa Juni 3, al-Sisi alitangazwa
rasmi kuwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho kwa asilimia 96.91 ya kura.
Uchaguzi huo umefanyika takriban mwaka mmoja baada ya
al-Sisi kuongoza mapinduzi dhidi ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia, Muhammed
Mursi, Julai 2013.
Chama cha Musri cha Udugu wa Kiislamu na makundi mengine
yanayopigania demokrasia nchini humo yaligomea uchaguzi huo, hatua
iliyosababisha kushuka kwa kiwango cha ushiriki wa wapiga kura.
Operesheni za jeshi dhidi ya wafuasi wa Mursi
zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 1,400 na maelfu kufungwa jela huku mamia
ya wafuasi wake wakihukumiwa kifo.
Ushindi wa al-Sisi unairudisha Misri mikononi mwa
kiongozi wa kijeshi miaka mitatu baada ya maandamano yalimng’oa Mubarak, ambaye
alikuwa ofisa wa jeshi la anga na aliyeitawala nchi hiyo kwa takribani miongo
mitatu.
0 comments:
Post a Comment