Rais mteule wa Misri, Abdulfattah al-Sisi |
Tume ya uchaguzi
nchini Misri imemtangaza rasmi mkuu wa zamani wa jeshi la nchi hiyo, Abdul
Fattah al-Sisi, kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika hivi karibuni
nchini humo.
Tume hiyo
imetangaza kuwa al-Sisi ameshinda kwa asilimia 96.1 ya kura zote zilizopigwa.
Aidha, tume
hiyo imesema kuwa waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 47.5 ya watu milioni 53 wenye sifa za kupiga kura. Hata hivyo,
baadhi ya vyama na mirengo ya upinzani imesema kuwa waliojitokeza kupiga kura
hawazidi asilimia 11.
Katika kinyang’anyiro
hicho al-Sisi alimshinda mpinzani wake pekee Hamdeen Sabahi ambaye ameukosoa
uchaguzi huo akisema kuwa ulikosa viwango.
Katika taarifa
yake ya Mei 28, kampeni ya Sabahi ilitangaza kuwaondosha mawakala wake wa
uchaguzi kwa sababu walikuwa wakitekwa au kushambuliwa.
"Ndani ya
saa 48 zilizopita tumekuwa tukilengwa kwa kudhalilishwa, kushambuliwa na kuvunjiwa
heshima. Mawakala wetu wamekuwa wakizuiliwa kuingia kwenye vituo vya kupigia
kura, wamekuwa wakishambuliwa na kukamatwa,” ilisema taarifa hiyo.
Uchaguzi ulihitimishwa
Mei 28 na kulazimika kuongezwa siku za upigaji kura kufuatia ushiriki mdogo wa wananchi.
Vuguvugu maarufu
la Udugu wa Kiislamu na makundi mengine yanayopigania haki za kidemokrasia
yaligomea uchaguzi huo, hatua iliyosababisha ushiriki mdogo wa wapiga kura
kuliko ule uliomuweka madarakani Rais aliyeondolewa, Muhammad Mursi.
Ushind wa al-Sisi
umeiweka Misri mikono mwa kiongozi wa kijeshi miaka mitatu baada ya maandamano
makubwa yaliyomuondoa Husni Mubarak ambaye alikuwa askari wa anga aliyeiongoza
nchi hiyo kwa miongo mitatu.
0 comments:
Post a Comment