AFGHANISTAN INAWEZA KUISHAMBULIA PAKISTAN

Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai


Afghanistan imetishia kuvishambulia vikosi vya Pakistan iwapo hawataacha kurusha makombora kwenye vijiji vya Afghanistan.

Waziri wa Ulinzi wa Afghanistan, Jenerali Bismillah Khan Mohammadi amesema kuwa vikosi vya nchi yake viko tayari kuchukua hatua dhidi ya askari wa Pakistan iwapo askari hao hawatoacha mara moja kurusha makombora kwenye vijiji vya vya nchi yake vinavyopakana na Pakistan.

Hata hivyo, Jenerali Mohammadi, aliwaambia wabunge kuwa jeshi la nchi hiyo halitachukua hatua hiyo bila kupata amri ya serikali ya kujibu mapigo.

Onyo hilo limekuja katika wakati ambao mivutano baina ya mataifa hayo mawili umepanda katika miezi ya hivi karibuni kuhusu mashambulizi ya mpakani.

Maafisa wa Afghanistan wanasema kuwa kwa uchache watu sita wameuawa na wengine 40 kujeruhiwa kutokana na makombora yanayorushwa kutoka upande wa Pakistan katika siku za hivi karibuni.

Aidha, jana serikali ya Afghanistan ilionya kuwa itajiondoa kwenye mazungumzo kuhusu ulinzi yanayoendelea baina ya mataifa hayo mawili kutokana na kulituhumu jeshi la Pakistan kuwa limekuwa likifanya mashambulizi hayo.

Maafisa wa usalama kutoka upande wa Afghanistan wameshasema kuwa hawatashiriki katika mkutano wa kikanda kuhusu usalama uliopangwa kufanyika Juni 4 mjini Islamabad, Pakistan.

Mnamo Mei 27, zaidi ya makombora 300 yalirushwa kutoka upande wa Pakistan na kutua katika maeneo mbalimbali ndani ya Afghanistan.


Mapema mwezi Mei, afisa usalama mmoja wa Pakistan alipoteza maisha kutokana na risasi zilizotoka upande wa Afghanistan katika mkoa wa milimani wa Bajaur, jambo ambalo limezidisha mivutano baina ya mataifa hayo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment