Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum |
Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum,
amewataka Waislamu nchini kuacha kumshambulia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kwa tofauti za kiitikadi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam
jana, Sheikh Alhad alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na
propaganda zinazowataka Waislamu kumchukia Lukuvi bila sababu za msingi.
Alisema hatua hiyo imewafanya baadhi ya waumini kuomba dua
maalumu dhidi ya Lukuvi bila kutambua msingi wa hoja hiyo.
Kwa mujibu wa Sheikh Alhad, chuki dhidi ya Lukuvi
inadaiwa kutokana na kauli yake ya kupinga serikali tatu kwa kuwa pamoja na
mambo mengine, haina vyanzo vya mapato, jambo ambalo linaweza kuiweka sehemu
mbaya na pengine hata kuchukuliwa na jeshi. (Pamoja na mambo mengine, Lukuvi anadaiwa kusema kuwa Zanzibar ikijitenga itakuwa nchi ya Kiislamu).
“Tunasema hivyo baada ya kugundua kuwa kuna kundi fulani
la Waislamu, ambao ni wafuasi wa chama kimoja cha siasa, ambao wamelibeba suala
la hotuba ya Lukuvi kwa mrengo ya kisiasa unaowanufaisha.
“Waislamu tukumbuke kuwa dini yetu inatufundisha kuwa
kumchukia mtu kusitufanye kutomtendea haki. Hivyo, ni vizuri tukamtendea haki
hata kama hatokani na chama chako unachokipenda au si muumini wa dini yako.
“Tunawaomba Waislamu kutokubali kutumiwa na vyama vya
siasa kwa maslahi binafsi, jambo ambalo linaweza kusababisha chuki miongoni
mwetu pasipo na sababu za msingi,” alisema.
Akizungumzia suala la Zanzibar kuwa dola ya Kiislamu,
alisema Lukuvi aliwasaidia Waislamu kujua wasiwasi walionao viongozi wa
Serikali kuhusu Zanzibar na kwamba huo ndio mrengo wa wanaotaka kujitenga kwa
kuachana na Tanzania Bara.
“Mimi sioni dhambi kama Wazanzibar watajitenga na kuwa
nje ya Muungano na kuanzisha dola ya Kiislamu nje ya Muungano,” alisema.
Katika hatua nyingine aliwataka viongozi wa UKAWA kurudi
katika meza ya majadiliano pamoja na wenzao wa chama tawala ili kukubaliana
kukamilisha mchakato wa Katiba.
Alhad alisema kilichofanywa na UKAWA kutoka kwenye vikao
vya Bunge Maalum la Katiba na kwenda kwenye mikutano ya hadhara, hakutasaidia
kupatikana kwa katiba mpya.
Alisema hatua hiyo itachochea vurugu na uvunjifu wa mani
ya nchi, jambo ambalo si vizuri kuliacha liendelee.
CHANZO: UHURU
0 comments:
Post a Comment