Waziri Mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra (katikati) akitoka nje ya Mahakama ya Katiba mjini Bangkok, jana Mei 6, 2014 alikokwenda kutoa utetezi wake. |
MAHAKAMA ya Katiba nchini Thailand imemuondosha
madarakani Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bi. Yingluck Shinawatra kwa kosa la
matumizi mabaya ya madaraka.
Mahakama hiyo imetoa hukumu leo kuwa Yingluck alitenda
kinyume na sheria alipomhamisha Mkuu wa Baraza la Usalama la Taifa Thawil
Pliensri kumpeleka kwenye wadhifa mwingine mwaka 2011.
Katika hukumu hiyo iliyokuwa ikitangazwa moja kwa moja
katika vituo vya televisheni, jaji Charoon Intachan alisema: “Wadhifa wake wa
uwaziri mkuu umekoma… Yingluck hawezi tena kuendelea na wadhifa wake kama Waziri
Mkuu.”
Hukumu hiyo imekuja siku moja baada ya Yingluck kufika
mahakamani na kupinga mashitaka yote yaliyofikishwa mbele ya mahakama hiyo.
“Ninazikataa tuhuma hizi… sikuvunja sheria, sikuwa na
maslahi yoyote katika uteuzi huo,” aliiambia mahakama hapo jana.
Mawaziri kadhaa katika baraza lake wanaweza kuondolewa
katika nyadhifa zao kwa tuhuma za kuunga mkono uamuzi wa Yingluck wa kumhamisha
Pliensri.
Wapinzani wanasema kuwa uhamisho wa Pliensri ulipangwa
ili kukinufaisha chama cha waziri mkuu kijulikanacho kwa jina la Puea Thai Party (PTP). Alirejeshwa katika
wadhifa wake mapema mwaka huu.
Kwa mujibu wa sheria za Thailand, naibu waziri mkuu
anaweza kukaimu nafasi ya waziri mkuu mpaka serikali mpya itakapoundwa baada ya
uchaguzi mwingine.
Hata hivyo, kuna uwezekano wa mahakama kuwatimua
mawaziri wengine, jambo ambalo litaifanya nchi kutokuwa na baraza la mawaziri
na bunge ambalo lilivunjwa mapema mwaka huu ili kupisha uchaguzi ambao baadae
ulibatilishwa.
Maandamano dhidi ya serikali yalizuka baada ya Oktoba
mwaka jana serikali kupeleka bungeni muswada ambao ungetoa msamaha kwa kaka wa Yingluck
na ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Thaksin Shinawatra, na
kumuandalia mazingira ya kurejea nchini Thailand. Zaidi ya watu 20 waliuawa
katika maandamano hayo.
Wapinzani wanamuona Yingluck kama kibaraka anayetumiwa
na kaka yake, ambaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya mwaka 2006. Waziri
Mkuu huyo wa zamani amekuwa akiishi uhamishoni tangu mwaka 2008 kwa kukwepa adhabu
ya kifungo cha miaka miwili jela aliyohukumiwa na mahakama ya nchi hiyo.
0 comments:
Post a Comment