Mkuu wa zamani wa jeshi la Misri na mgombea wa kiti cha urais wa nchi hiyo Abdul-Fattah al-Sisi. |
KAMPENI za uchaguzi wa urais nchini Misri zimeanza rasmi
muda mfupi baada ya mashambulizi mabaya ya mabomu na ghasia kuyagharimu maisha
ya watu kadhaa nchini humo.
Kampeni hizo zimeanza rasmi leo na zinatarajiwa
kumalizika Meo 23 ambapo uchaguzi utafanyika Mei 26 na 27 mwaka huu.
Jana milipuko miwili ya mabomu katika Peninsula ya Sinai
na katika mji mkuu, Cairo, iliwaua watu wasiopungua watano, huku wengine kadhaa
wakipoteza maisha katika ghasia za makabiliano baina ya vikosi vya usalama na
waandamanaji wanaoipinga serikali.
Mkuu wa zamani wa jeshi la nchi hiyo, Abdul Fattah al-Sisi,
anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo.
Itakumbukwa kuwa Julai mwaka jana al-Sisi alitangaza
kumuondosha madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Muhammad Mursi.
Mshindani pekee wa al-Sisi katika kinyang’anyiro hicho
ni Hamdeen Sabbahi, ambaye alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa mwaka
2012 uliomuingiza Mursi madarakani.
Serikali ya nchi hiyo imekuwa katika mzozo mkubwa na
wafuasi wa Mursi tangu kuondolewa kwake madarakani Julai mwaka jana.
Makundi ya haki za binadamu yanasema kuwa tangu wakati
huo zaidi ya watu 1,400 wameuawa na maelfu kutupwa gerezani.
Serikali ya sasa inayoungwa mkono na jeshi ililitangaza
vuguvugu la Udugu wa Kiislamu kuwa kundi la kigaidi huku ikitangaza operesheni
kubwa ya kukabiliana na wafuasi wa vuguvugu hilo.
Zaidi ya wafuasi na wanachama 1,000 wa vuguvugu hilo
wameshahukumiwa adhabu ya kifo mwaka huu pekee.
0 comments:
Post a Comment