Aliyekuwa mkuu wa jeshi la Sudan Kusini Jenerali James Hoth Mai |
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amemfuta kazi mkuu wa
jeshi la nchi hiyo kufuatia eneo muhimu la mafuta kuangukia mikononi mwa waasi
wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo, Riek Machar.
Kituo cha Televisheni ya serikali ya nchi hiyo
kimetangaza kuwa Jenerali James Hoth Mai amefutwa kazi na nafasi yake
kuchukuliwa na Jenerali Paul Malong.
Rais hajatoa sababu ya kumuondosha Hoth Mai, lakini duru
za ndani zinasema kuwa hatua hiyo inatokana na tukio la hivi karibuni kwa jeshi
hilo kupoteza eneo muhimu la mafuta kaskazini mwa nchi.
Wiki iliyopita, vikosi vya waasi viliutwaa mji wa Bentiu,
ambao ni mji mkuu wa jimbo lenye utajiri wa mafuta la Unity,na kudaiwa kufanya
mauaji makubwa ya kikabila.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mamia ya wananchi
waliuawa wakati waasi walipokuwa wakiwawinda wananchi waliokuwa wakitafuta
hifadhi misikitini, makanisani na hospitalini.
Umoja huo unasema kuwa waasi walitumia matangazo ya
redio kuibua hisia za kikabila katika eneo hilo.
Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko Desemba 2013, baada
ya mapigano kuzuka mjini Juba baina ya askari watiifu kwa Rais Kiir na wale
wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wake, Machar.
Muda mfupi baadaye mgogoro huo uliibuka kuwa vita vya
jumla kati ya jeshi na wale waasi, huku ghasia hizo zikichukua mkondo wa
kikabila baina ya kabila la Rais la Dinka na lile la Machar la Nuer.
Mwezi
Januari mwaka huu pande hizo mbili zilisaini makubaliano ya kusitisha mapigano
lakini yalizuka tena katika maeneo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.
Mgogoro huo umesababisha vifo vya maelfu ya raia na
wengine wapatao milioni moja kulazimika kuyakimbia makazi yao.
Sudan Kusini ilipata uhuru wake Julai 2011baada ya
wananchi wa eneo hilo kupiga kura kujitenga na Sudan Kaskazini.
0 comments:
Post a Comment