ROUHANI: URUTUBISHAJI WA URANI NDANI YA IRAN NI MSITARI MWEKUNDU





Na Kabuga Kanyegeri


RAIS wa Iran, Hassan Rouhani amelielezea suala la urutubishaji wa madini ya urani ndani ya Iran kuwa ni “msitari mwekundu” kwa nchi yake.

Rouhani ameyasema hayo kufuatia mazungumzo baina ya Tehran na mataifa mataifa makubwa yaliyofanyika hivi karibuni mjini Geneva.

“Kwetu sisi, mstari mwekundu ni marufuku kwa mtu yeyote kuuvuka. Haki na maslahi ya Iran ni mstari mwekundu kwetu; na haki hizo zinajumuisha haki za kuwa na nishati ya nyuklia ndani ya utaratibu na sharia za kimataifa, na pia urutubishaji wa urani ndani ya ardhi ya Iran,” alisema Rouhani wakati akilihutubia bunge la nchi hiyo leo.

Rouhani alifika bungeni kumtetea mteule wake wa nafasi ya Wizara ya Vijana na Michezo, Nasrullah Sajjadi. Kwa mujibu wa katiba ya Iran, mawaziri wanaoteuliwa na rais wanalazimika kuhojiwa na kupitishwa na Bunge la nchi hiyo, Majlis.

Rais huyo wa Iran alisisitiza kuwa “vikwazo, vitisho, hila na ubaguzi” havitakuwa suluhisho katika kuamiliana na taifa lake.

“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijapiga magoti na haitapiga magoti mbele ya vitisho vyovyote,” alisema.

Mapema leo, Iran na mataifa matano yenye uanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa – Uingereza, Ufaransa, China na Marekani – pamoja na Ujerumani, walihitimisha mazungumzo ya siku tatu juu ya programu ya nyuklia ya nchi hiyo.

Rouhani alitupilia mbali madai kuwa vikwazo ilivyowekewa Tehran na Jumuiya ya Kimataifa viliilazimisha kutaka suluhu na mataifa makubwa. Bali imekuwa ikifanya hivyo tokea zamani, hata kabla ya vikwazo, kwa kuwa siku zote imekuwa muumini wa utatuzi wa masuala mazito kwa njia ya mazungumzo badala ya vitisho.

Marekani, Israeli na waitifaki wao wamekuwa wakiituhumu Iran kwamba inarutubisha madini ya urani kwa ajili ya kutengeneza silaha za nyuklia, jambo lililoisukuma Marekani na Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo vya kiuchumi. Hata hivyo, Tehran imekuwa ikikanusha madai hayo na kusema kuwa program yake inalenga kutumia teknolojia ya nyuklia kwa miradi ya kijamii na ya amani.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment