Hatimaye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zitto Zuberi Kabwe, ametoa tamko rasmi dhidi ya kile kinachoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema" inayomhusisha na kukihujumu na kukivuruga Chama hicho. Hii ndiyo taarifa yake akijibu madai na tuhuma hizo, sanjari na kueleza hatua atakazozichukua:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMKO rasmi la Ndugu Zitto Z. KABWE (MB) kuhusiana na
kinachoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema"
Ndugu Wanahabari,
NILIPOKUWA katika ziara ya bara la Ulaya kati ya Oktoba
21 mpaka Novemba 2 mwaka huu (2013), nilipokea kwa njia ya barua pepe ripoti
inayoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema" ambayo pia ilikuwa imesambazwa
katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama
changu) kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na
kubaini kuwa mimi napokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga
Chadema.
Ripoti hiyo ilinihusisha pia na mwananchi raia wa
Ujerumani, Andrea Cordes ambaye, kwa mujibu wa ripoti hiyo, alinisaidia kupokea
na kuhifadhi kiasi cha dola 250,000 za Marekani kupitia kwenye akaunti yake
binafsi.
Taarifa hii ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha
kutisha, imenifadhaisha, kunisikitisha na kunikasirisha.
Taarifa hii iliibuliwa katika kipindi ambacho nilikuwa
safarini kutetea haki za Watanzania na Waafrika ambao utajiri wao wa rasilimali
unafaidiwa na watu wachache waliohifadhi mali katika nje za nje na pia
kupigania makampuni ya mataifa tajiri yalipe kodi stahiki katika nchi zetu.
Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka
kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania
wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa
taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu.
Nafahamu kwamba mimi ni mwanasiasa ambaye nimekuwa
mlengwa (target) wa mashambulizi kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanasiasa na
vikundi vyao. Kama mwanasiasa, niko tayari kupokea changamoto zozote zinazokuja
na uanasiasa wangu.
Hata hivyo, ambacho sitakubali ni kwa watu kutumia jina
langu na uanasiasa wangu kunichafua mimi binafsi na watu wengine wasiohusika
kwa sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.
Raia huyo wa Kijerumani tayari amekana kuhifadhi fedha
zangu. Kwa maelezo yake kwa baadhi ya viongozi wa Chadema amekana kuwa na
akaunti inayotajwa na amekana pia kuwepo nchini Ujerumani katika siku na wakati
uliotajwa kwenye ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imemtaja pia mtu kama Dk. Charles Kimei,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB ikidai kwamba nilikutana naye na
alishiriki kwenye igizo hilo la kunipa fedha.
Niseme mapema kwamba tangu kuzaliwa kwangu sijawahi hata
mara moja kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani au nje ya nchi. Kumuingiza
mtu ambaye amejenga jina lake kwenye taaluma ya kibenki kwa sababu tu ya lengo
ovu la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si uungwana bali ni unyama.
Kutokana na uchafuzi huu wa wazi dhidi ya taswira yangu
binafsi na watu wengine walioingizwa kwenye mkumbo huu, nimeandika rasmi kwa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa kumwomba athibitishe kwamba kinachoitwa
Taarifa ya Siri ya Chadema ni kweli ni taarifa ya chama au kiikanushe ili
niweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa hekaya hiyo.
Cha ajabu, nimepokea ujumbe wa kutishiwa maisha kutoka
kwa mtu anayejiita Theo Mutahaba na kuahidiwa KUPOTEZWA endapo nitaendelea na jitihada
zangu za kupambana na ufisadi na kutafuta haki kwa Watanzania wote pasipo
kujali tofauti zao za kiitikadi, kikanda, kikabila na kidini.
Natarajia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote
ambao wamehusika na utungaji na uenezi wa taarifa hii. Nitahakikisha kwamba
wahusika wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka stahiki ya upotoshaji na
kuchafuana.
Ni matarajio yangu kwamba wale wenye mapenzi mema na
Tanzania, mimi binafsi na utawala wa sheria, wataelewa nia yangu ya kutafuta
haki katika suala hili.
Nimeamua kujitolea maisha yangu kwa ajili ya Watanzania
na kama alivyopata kusema Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela;
“Struggle Is My Life.”
Forward Ever, Backward Never- Kwame Nkrumah
Zitto Kabwe (Mb)
10/11/2013
.jpg)
0 comments:
Post a Comment