LIBYA YAENDELEA KUMEGUKA: MASHARIKI YAJITANGAZIA SERIKALI YAKE

 


Na Kabuga Kanyegeri


Eneo la mashariki mwa Libya lenye utajiri wa mafuta limeitangazia serikali yake, katika hatua ambayo inaweza kutafsiriwa kama changamoto kwa serikali kuu ya taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika.

Jana Jumapili, viongozi wa vuguvugu lililojitenga walikutana katika mji wa Ajdabiya na kuizindua rasmi serikali yao chini ya jina la Barqa au Cyrenaica. Katika sherehe hizo, zaidi ya mawaziri 20 walioneshwa katika televisheni wakila kiapo.

Tangazo hilo ni pigo kwa serikali ya Tripoli ambayo imekuwa ikijaribu kuzifungua upya bandari za eneo la mashari lenye utajiri mkubwa wa mafuta ambazo zilifungwa kutokana na migogoro ya uasi na migogoro ya kikabila, ambapo makundi hayo yanataka kupata fungu kubwa la madaraka na mapato ya mafuta.

Aidha, hatua hiyo itazorotesha uhusiano kati ya mashariki na Tripoli, ambayo imepinga vikali hatua hiyo.

Viongozi wa eneo la mashariki wanamtuhumu Waziri Mkuu wa Libya, Ali Zeidan na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Kitaifa kwa ufisadi na kushindwa kuimarisha usalama tangu kuanguka kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi.

Uzalishaji wa mafuta nchini Libya umeshuka kwa asilimia 10 ya uwezo wake wa kuzalisha mapipa milioni 1.25 kwa siku kutokana na maandamano na migomo kwa bandari na viwanda vya uzalishaji mafuta.


Eneo la mashariki limekuwa likikumbwa na matukio mbalimbali ya ghasia na vurugu, ambapo askari mmoja aliuawa na mwingine kujeruhiwa baada ya mgodi mmoja kulipuka jirani na kizuizi cha jeshi katika mji wa Benghanzi juzi Jumamosi.

Katika tukio jingine, mlipuko wa bomu ulimuua afisa upelelezi na binti yake katika mji huo.

Watu wapatao 100 walikusanyika katika mji huo kupinga mauaji hayo wakiituhumu serikali ya Libya na bunge kwa kushindwa kuimarisha usalama.


Tangu kuangushwa na kuuawa kwa Gaddafi mwaka 2011, serikali ya Libya imekuwa ikikabiliana na uwepo wa wapiganaji wenye silaha, ambao walishiriki katika mapambano dhidi ya utawala wa Gaddafi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment