MURSI AFIKISHWA MAHAKAMANI LEO





Na Kabuga Kanyegeri

RAIS aliyeondolewa mdarakani nchini Misri, Muhammad Mursi, leo amepelekwa mahakamani mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Cairo, kujibu mashitaka ya mauaji anayodaiwa kuyafanya katika kipindi cha uongozi wake uliodumu kwa muda wa mwaka mmoja.

Mursi ambaye ni kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo aliwasili leo kwenye mahakama iliyoko katika chuo cha polisi.

Mursi anakabiliwa na mashitaka ya kuchochea ghasia na mauaji yanayohusisna na vurugu zilizotokea nje ya ikulu mwezi Desemba 2012. Iwapo atapatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifo au kifungo cha maisha gerezani.

Maafisa kumi na nne wa Vuguvugu la Udugu wa Kiislamu, wakiwemo wasaidizi watatu wa Mursi, nao watafika mahakamani leo.

Vuguvugu la Udugu wa Kiislamu limeyaelezea mashitaka hayo kuwa yametengenezwa na kuwataka wafuasi wake kumiminika mitaani kupinga hatua hiyo. Mpaka tunaandaa taarifa hii, mamia kwa maelfu ya wafuasi hao wameitikia wito huo.

Muungano wa makundi yanayopinga mapinduzi ya kijeshi yaliyomng’oa Mursi madarakani, umeeleza kuwa hautashirikiana na mamlaka za serikali kwa sababu Mursi haitambui mamlaka ya mahakama hiyo.

Jana Jumapili, mamlaka zilibadilisha eneo la kuendeshea kesi hizo kwa hofu ya kuibuka ghasia na umwagikaji wa damu. Uamuzi huo wa dakika za mwisho ulifanyika baada ya wafuasi wa Mursi kuitisha maandamano makubwa nje ya eneo la awali.

Mnamo Julai 3, mkuu wa jeshi la Misri, Jenerali Abdul Fattah al-Sisi, alimuondoa Mursi madarakani. Baadaye rais huyo alikamatwa na kupelekwa mahali kusikojulikana.

Mnamo Novemba 1, maelfu ya wananchi waliandamani nchi nzima wakipinga mashitaka dhidi ya Mursi na kutaka arejeshwe madarakani. Aidha, walitaka kuwajibishwa kwa wale waliohusika na mauaji ya wafuasi wa Mursi tangu Julai 3.

Idadi kubwa ya maafisa na wafuasi wa Vuguvugu la Udugu wa Kiislamu wanashikiliwa korokoroni.


Mashitaka hayo yanakuja muda mfupi baada ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, mjini Cairo. Kerry amekutana na viongozi wakuu wa Misri, ambapo aliahidi Washington kuiunga mkono serikali ya mpito ya nchi hiyo. 
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment