DK SEZIBERA: MGOGORO AFRIKA MASHARIKI UTAJADILIWA NA MAWAZIRI


Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Richard Sezibera

BAADA ya kimya juu ya mgogoro wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hatimaye Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk Richard Sezibera, ameibuka na kusema kuwa mgogoro miongoni mwa nchi wanachama utajadiliwa kwa kina katika kikao kijacho cha Baraza la Mawaziri.

Kikao hicho cha mawaziri, kwa mujibu wa Dk Sezibera, kitafanyika Novemba 28 mwaka huu. Kikao hicho ndicho kikao cha juu ambacho kinatoa mapendekezo mbalimbali yanayoenda kujadiliwa kwenye vikao vya wakuu wa nchi wanachama.

Dk Sezibera ambaye ni raia wa Rwanda, ndiye anayeongoza Sektarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye makao yake makuu mjini Arusha na alikuwa hajasema lolote tangu kuanza utaratibu wa nchi tatu kukutana bila kushirikisha Tanzania na Burundi na wala haijajibu malalamiko ya Serikali ya Tanzania.

Katika taarifa yake, Katibu Mkuu huyo alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa nchi za Burundi na Tanzania kuhusu wasiwasi wa vikao kadhaa vilivyofanywa na viongozi wakuu wa nchi za Kenya, Rwanda na Uganda bila kuwashirikisha wanachama wenzao.

Kwa muda sasa muungano huo haramu wa nchi tatu umekuwa unaripotiwa kwa kina na vyombo vya habari kuhusu kutengwa kwa nchi hizo mbili, lakini sektarieti hiyo iliendelea kukaa kimya.

Tanzania ilitoa tamko la wazi kuwa nchi hizo zimekiuka makubaliano yaliyoko kwenye mkataba wa jumuiya hiyo.

“Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ameshauriana na nchi tano wanachama kuhusu suala hilo,” alisema Dk Sezibera na kuongeza kuwa katika mkutano wa 19 wa Baraza la Mawaziri wa kisekta, alibadilishana mawazo na mawaziri na wote walionesha nia ya kuendelea kujenga jumuiya hiyo, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zilijitokeza.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu huyo amewaomba wananchi wa Afrika Mashariki wasishtushwe na changamoto zilizojitokea, kwani zinashughulikiwa na zitajadiliwa kwa kina katika mkutano wa mawaziri ambao utafanyika Novemba 28 na utatoa mapendekezo juu ya kilichojiri kwenye mkutano huo.

Alisema nchi wanachama zimedhamiria kuanza utekelezaji wa itifaki za soko la pamoja na ushuru wa forodha, ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa miundombinu, kuondoa vikwazo kwenye usafirishaji wa mizigo ya biashara, huduma na watu.

Rais Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya juzi walikutana tena mjini Kigali, Rwanda, pamoja na mambo mengine, walitarajia kusaini makubaliano ya kuanzisha kituo kimoja cha kukusanya ushuru kinachotarajia kurahisisha uchukuzi wa bidhaa kutoka Mombasa nchini Kwenya, Uganda hadi Rwanda.

Katika mkutano huo, Rais Salva Kiir wa Sudan alialikwa kama mshirika. Mkutano huo ulifanyika baada ya ule uliofanyika mjini Kampala Uganda, Juni mwaka huu na mwingine uliofanyika Mombasa, Agosti, ambako viongozi hao watatu walipendekeza kupanuliwa kwa Bandari ya Mombasa, ili kuwezesha uharaka wa bidhaa kupitishwa katika kuhudumia Kanda nzima.

Hivi karibuni, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alitangaza kuwa Tanzania itatoa ‘talaka’ kwa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambazo zimeamua kuanzisha Jumuiya ya hiari nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Sitta alisema kutokana na nchi hizo kuonekana kuitenga Tanzania na Burundi ambazo ni wanachama wa jumuiya hiyo, wameshaanza mazungumzo ya kushirikiana kiuchumi, kisiasa na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC).


“Hawa wenzetu wanafanya utoto wa kutuzunguka, sisi tunatumia hekma za mzee Mwinyi alieyesema ‘mwongo, mwongoze’. Kama wao wana hila zozote juu yetu, siku si nyingi tutazibaini, kama ndoa kwenye jumuiya basi sisi ndio tutakuwa tumeoa… hivyo tutatoa talaka wakati wowote,” alisema Sitta baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi na Wabunge.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment