| Waasi wa M23 wakitembea msituni katika jimbo la Kivu Kaskazini |
Kiongozi wa kundi la waasi la M23 la nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Bertrand Bisimwa, ametaka kusimamishwa mapigano na
vikosi vya serikali katika jaribio la kutaka kuendeleza mazungumzo ya amani na
serikali ya Kongo.
Bisimwa amesema kuwa lengo lake ni “kuruhusu muendelezo
wa mchakato wa kisiasa” na wasimamizi wa mazunguzo ya amani yanayoendelea
nchini Uganda.
Hili limekuja baada ya Uganda kutoa wito wa kusimamishwa
kwa mgogoro uliodumu kwa takriban miezi 20 baina ya jeshi la Kongo na waasi wa
M23.
Tangu Jumatano, Kampala imekuwa mwenyeji wa awamu mpya
ya mazungumzo ya amani, siku kumi baada kuvunjika kutokana na waasi wa M23
kuweka sharti la kusamehewa kwa viongozi wao wote.
Roger Lumbala, mwakilishi mkuu wa M23 kwenye mazungumzo
hayo, alisema kuwa waasi walikuwa tayari kusaini mkataba wa amani iwapo
wangepokea mwaliko kutoka kwa wasimamizi wa mazungumzo hayo.
Hata hivyo, jeshi la Kongo liliapa kuyafutilia mbali
makundi yote ya waasi.
Makundi kadhaa yenye silaha, ikiwemo M23, wanaendesha
harakati zao za uasi mashariki mwa Kongo na wanapigania kuidhibiti nchi hiyo
kubwa yenye maliasili za madini, kama vile dhahabu, urani, coltan, ambayo
hutumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya elektroniki, ikiwemo simu za
mkononi.
Waasi wa M23 walijiondoa katika jeshi la Kongo mwezi
Aprili 2012 kupinga kile walichodai kuwa ni mwenendo mbaya ndani ya jeshi la
Taifa (FARDC). Walikuwa wamejumuishwa katika jeshi chini ya mkataba wa amani
uliosainiwa mwaka 2009.
Tangu mwezi Mei 2012, takriban watu milioni 3
wameyekimbia makazi yao katika eneo la mashariki mwa Kongo. Takriban watu
milioni 2.5 ni wakimbizi wa ndani, huku zaidi ya watu 460,000 wamekimbilia
katika nchi za Rwanda na Uganda.
Kongo imekuwa ikikabiliwa na matatizo matatizo kwa
miongo kadhaa, kama vile umaskini uliokithiri, miondombinu mibovu, na vita
katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambavyo viliibuka tangu mwaka 1998 na
kugharimu maisha ya zaidi ya watu milioni 5.5.
0 comments:
Post a Comment