| Picha ikionesha hali halisi baada ya Kimbunga Haiyan katika mji wa Tacloban, kwenye kisiwa cha Leyte Novemba 9, 2013. |
Na Kabuga Kanyegeri
MAAFISA wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Ufilipino
wanasema kuwa kwa uchache watu wapatao 1,200 wamepoteza maishha baada ya
kimbunga Haiyan kuyapiga vibaya maeneo mawili nchini humo na kusababisha
gharika kubwa kuikumba nchi hiyo inayopatikana Kusini Mashariki mwa bara la
Asia.
Katibu Mkuu wa shirika hilo nchini Ufilipino, Gwendolyn
Pang, amesema kuwa idadi hiyo ya vifo ilitokana na ripoti za awali za wafanya
kazi wa shirika hilo waliokuwa wakistoa huduma mbalimbali za kibinaadamu.
Aidha, duru zinasema kuwa idadi ya vifo inatarajiwa
kuongezeka wakati vikosi vya usalama vitakapoyafikia maeneo ya ambali ambayo
yameharibiwa vibaya sana na kimbunga hicho kinachokwenda kwa kasi.
Zaidi ya Wafilipino milioni moja wamelazimika kuyakimbia
makazi yao na kukimbilia maeneo salama.
Haya yanatokea baada ya Kimbunga Haiyan, ambacho ni
miongoni mwa vimbunga vikubwa mno kuwahi kutokea, kukipiga kisiwa cha mashariki
cha Samar kabla ya kwenda katika visiwa vingine vitano.
Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa miongoni mwa
maeneo yaliyoathiriwa vibaya ni kisiwa cha Leyte kilichopo mashariki mwa nchi
hiyo na pwani ya mji wa Tacloban, ambako majengo yamebomolewa na miti kung’olewa.
Kimbunga hicho pia kilisababisha mmomonyoko wa udongo, mafuriko na kukata umeme
na mawasiliano katika visiwa kadhaa.
Aidha, kimbunga hicho kinatarajiwa kusababisha mvua
katikati mwa nchi ya Vietnam kesho Jumapili. Pia, kinatarajiwa kusonga mbele na
kuyaathiri vibaya maeneo ya pwani ya kusini mwa China.
Kwa mujibu wa maafisa, zaidi ya watu milioni 12 wapo katika
hatari ya kuathiriwa na kimbunga hicho kikali.
Wastani wa vimbunga 20 huipiga nchi ya Ufilipino kila mwaka.
Mwezi Desemba mwaka 2011, Kimbunga Washi kilisababisha vifo vya watu 1,200,
kuwahamisha watu 300,000 na kuyaharibu zaidi ya makazi 10,000.
Mwaka jana kimbunga Bopha kilipiga katika miji mitatu ya
pwani kwenye kisiwa cha Mindanao, kikaua watu 1,100 na kusababisha uharibifu
unaokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani bilioni 1.04.
Mwezi Septemba, Kimbunga Usagi, kilichokuwa kikisafiri
kwa kasi ya kilometa 240 kwa saa, kilipiga katika kisiwa cha Batanes kilichopo
kaskazini mwa nchi hiyo kabla ya kusababisha hasara kubwa nchini China.
0 comments:
Post a Comment