WAZIRI Mkuu wa Libya, Ali Zeidan, ameripotiwa kuachiwa
saa kadhaa baada ya kutekwa na watu wenye silaha katika hoteli moja katika mji
mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.
Waziri wa Mambo ya nje wa Libya, Mohammed Abdelaziz amethibitisha
kuwa Zeidan ameachiwa huru.
Hata hivyo, waziri huyo alisema kuwa mpaka sasa hawana
taarifa za kina za mazingira ya kuachiwa kwake.
Taarifa hiyo inakuja saa chache baada ya vyanzo kutoka serikali
ya Libya kusema kuwa kundi moja la waasi wa zamani ndilo lililohusika na
kumteka na kumpeleka kusikojulikana.
Serikali ya Libya ililaani kitendo cha kukamatwa kwa
Waziri Mkuu na kukiita kuwa ni “kitendo cha kihalifu.”
Kundi moja la waasi wa zamani linalojulikana kama Operations
Cell of Revolutionaries (OCR) lilidai kuhusika na tukio hilo.
Kundi hilo liliandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa lilimkamata Zeidan kwa amri ya
waendesha mashitaka, lakini ofisi ya mwendesha mashitaka ilikanusha kutoa
kibali cha kukamatwa kwa Zeidan.
Utekwaji huo umefanywa siku kadhaa baada ya vikosi vya
Marekani kufanya shambulizi la kushitukiza mjini Tripoli na kumkamata mtu
anayedaiwa kuwa kiongozi wa al-Qaeda nchini humo, Abu Anas al-Libi.
Al-Libi, mwenye umri wa miaka 49, anaripotiwa kushikiliwa
na kuhojiwa katika meli ya kivita ya Marekani, USS San Antonio, ambayo imeweka
nanga baharini.
Serikali ya Libya inalichukuliwa shambulizi hilo la
Marekani kama utekaji nyara wa raia wa Libya, na wamemhoji balozi wa Marekani
nchini humo kuhusu hatua hiyo.
Mnamo Oktoba 8, Zeidan aliwaambia waandishi wa habari
mjini Tripoli kuwa, uhusiano wetu na Marekani ni muhimu, na tunalizingatia
hilo, lakini pia tunawajali raia wetu, na hilo ndio jukumu letu.”
0 comments:
Post a Comment