Waraka wenye vitisho ukiwa na nembo ya Jumuiya ya Uamsho
na mihadhara ya Kiislam (JUMIKI) umesambazwa visiwani hapa, ukidaiwa kutishia
kufanyika kwa shambulio dhidi ya viongozi wa dini na Serikali kabla ya Sikukuu
ya Eid El Haj.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam
Khamis Mkadam amethibitisha kupata nakala ya waraka huo wenye maneno makali na
vitisho kwa usalama wa watu na amani ya nchi. Kamanda Mkadam alisema,Polisi
imefanikiwa kuupata waraka huo baada ya tukio hilo kuripotiwa na baadhi ya
viongozi wa madhehebu za dini Visiwani humo.
Hata hivyo, alisema,tayari makachero wa Polisi wako
kazini na ametoa wito kwa viongozi wa dini na wananchi kuondoa hofu kwa vile
vyombo hivyo vya ulinzi na usalama vimejiandaa kukabiliana na tukio lolote la
kihalifu.
Aliwahi wananchi kuendelea na jitihada za kuwafichua
wahalifu na watu wanaowatilia shaka dhidi ya amani visiwani hapa.
“Hatua tulizochukua ni pamoja na kuwataka viongozi wa
dini kuanzisha kamati za ulinzi mbali na kuwapatia huduma za ulinzi kama njia
ya kukabiliana na matukio mbalimbali,”alisema Kamanda Mkadam.
Waraka huo unadaiwa kuainisha vitendo vya hujuma kuwa
vitazidi hadi pale Zanzibar itakapofanikiwa kurejesha kile kilichoitwa Uhuru
wake.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment