Kitambulisho cha Usalama wa Taifa, alichokuwa akitumia,
Bw. Magige, kwenye majukumu aliyokuwa akijipangia
|
Bw. Kennedy Magige, anayedaiwa kuwa Ofisa wa Idara ya
Usalama wa Taifa 'feki' akiwa hoi baada ya kunaswa na kupata kipigo kutoka kwa
wananchi.
|
Bw. Magige na mtuhumiwa mwenzake wakiwa kwenye gari la
Polisi tayari kupelekwa kituoni
|
Gari aina ya Land Cruiser Prado, alilokuwa akitumia
wakati wa shughuli zake za kila siku
|
Watu wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya
utapeli , huku mmoja akitumia kitambulisho kinachomtambulisha kuwa ni ofisa
mwandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa, wametiwa mbaroni jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo ambalo liligusa hisia za watu wengine
lilitokea juzi maeneo ya Kawe, wakiwa katika Hoteli ya Picol Beach saa 2.30
siku baada ya kuwekewa mtego.
Watuhumiwa hao watanashati waliokamatwa katika tukio
hilo wametambuliwa kuwa ni Fadhili Hamisi Mafutari ambaye anadaiwa kutumia
kitambulisho cha Idara ya Usalama wa Taifa, kikiwa na jina la Kennedy Magige na
picha yake.
Pia anatumia simu yenye namba 0654-084-445 iliyosajiliwa
kwa jina la Kennedy Magige, ingawa rafiki yake ambaye amekamatwa naye kwenye
tukio hilo, Tabula Abdallah Mayenga, alisema anamfahamu na jina lake, Fadhili
Hamisi Mafutari.
Watu hao walikamatwa baada ya kuwekewa mtego na watu
wanaodai kutapeliwa na Mayenga katika tukio lililotokea Ijumaa, wiki iliyopita
maeneo ya Maua Resort Beach.
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa mashuhuda alisema baada
ya kutapeliwa, walianza kuweka mtego na kufanikiwa kumnasa Magige, kwa kutumia
mtu mwingine aliyempigia simu na kujifanya ana shida naye.
Mtoa habari wetu huyo, alidai kwamba wakati Magige
anawafanyia tukio hilo la utapeli, hakuwa anafahamu k ama wamebaki na namba
yake simu na baada ya kufuatilia, walibaini imesajiliwa kwa jina la Magige.
"Alipopigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwake
pengine alidhani amekutana na mjinga mwingine, hivyo walipanga wakutane Hoteli
ya Picol Beach," alisema mtoa habari wetu.
Vyanzo vyetu hivyo, vilieleza kuwa Magige alifika
hotelini hapo akiwa na gari aina Land Cruiser Prado namba T445 BCY na kisha
kukutana na mtu aliyekuwa amepanga naye, bila kujua alikuwa anaingia mtegoni.
Baada ya kufika, alitiwa mbaroni pamoja na mwenzake na
kuanza kushushiwa kipigo kikali na wananchi wenye hasira, ambapo ilibainika
anamiliki kitambulisho kinachomtambulisha kuwa ni ofisa mwandamizi Idara ya
Usalama wa Taifa.
Lakini alipohojiwa, Magige alijitambulisha kuwa yeye ni
mfanyabiashara wa mazao aina ya nafaka kauli ambayo ilitofautiana na rafiki
yake ambaye alikamatwa naye kwenye tukio hilo, kwani alisema Mafutari (Magige)
ni mfanyabiashara wa magari.
Mayenga alisema yeye ni fundi seremala na kwamba alifika
hotelini hapo kufuata hela kidogo kwa rafiki yake,lakini ghafla aliona watu
wanaanza kumfuatilia na hakuwa na njia ya kukimbia kwani alihisi ataitiwa
mwizi.
Baada ya watu hao kupata kipigo kutoka kwa wananchi,
walifika Polisi ambao waliweza kubaini kitambulisho hicho cha usalama wa taifa,
lakini Magige alipohojiwa alikana kuwa si mali yake.
Watuhumiwa hao waliondolewa eneo la tukio kwa kutumia
gari la Polisi namba T 332 ANV aina ya Land Rover Difender.Akisimulia tukio la
kutapeliwa na mtu huyo, anayedaiwa kuwa usalama, shuhuda mmoja alisema akiwa na
dada yake Ijumaa iliyopita maeneo ya Maua Resort Beach, Kunduchi alifika mtu
huyo, ambapo alijifanya kama anawafahamu hivyo wakawa wamekaa wote.
Mtu huyo, alianza kuwauliza habari za siku nyingi yeye
na dada yake, wakati huo wakinywa soda. Alisema mtu huyo, inasemekana
aliwawekea kitu kinachodhaniwa ni dawa za kulevya kwenye kinywaji chao, kwani
hali zao zilibadilika.
Alisema dada yake huwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo,
hivyo ghafla alianza kuhisi miguu kumwishia nguvu, ndipo alipowaambia aende
kwenye gari yake ili apate kiyoyozi na walifanya hivyo.
Shuhuda huyo alisema Magige alianza kuwauliza kama wana
kadi za ATM, kwani yeye hana, lakini kuna mtu anataka kumtumia fedha kutoka
Arusha. Walipomwambia itawezekanaje muda huo usiku, aliambiwa kuwa Arusha
wanachelewa, ndipo walikataa na hapo kuanza kumtilia shaka.
Baada ya hapo, shuhuda huyo anaeleza kwamba alianza
kumpora dada yake vitu alivyokuwa navyo na kurudisha gari nyuma kwa kasi na
kuanza kuondoka na ndugu yake huyo. Alisema na yeye alikuwa na gari, hivyo
alianza kumfukuzia lakini alipofika maeneo ya Mtongani, aliishiwa nguvu, hivyo ilibidi
aende kutoa taarifa Polisi Mtongani.
Alisema mtuhumiwa huyo,alienda na dada yake hadi maeneo
ya hoteli moja (jina tunalo), ambapo alitaka kumtelekeza, lakini alipiga kelele
kuomba msaada ambapo walianza kulifukuza gari hilo kwa Bajaj, lakini alifanikiwa
kuwaacha, hivyo ndipo alipokumbuka namba na kuwapigia na kukutana nao Polisi,
Mtongani.
Alisema tangu wakati huo walianza kuweka mtego wa kunasa
matapeli hao, hadi jana walipotiwa mbaroni. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi
Kinondoni, Camillus Wambura, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, simu yake
ilikuwa inaita bila kupokewa.
CHANZO: MAJIRA/ JAMBO TANZANIA
0 comments:
Post a Comment