WATUHUMIWA 11 ambao walikamatwa wakifanya mafunzo yanayodaiwa
kuwa ya kigaidi kwa kutumia CD za Al Shabaab na Al Qaeda katika msitu wa
Makoloanga wilayani Nanyumbu, Mkoa wa Mtwara, jana walikwama kufikishwa
mahakamani kutokana na taratibu za kuwahamishia mkoani kutokamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, alisema kuwa wamewarudisha mahabusu wilayani
Nanyumbu watuhumiwa hao.
“Leo tulitarajia kuwafikisha watuhumiwa hawa wa ugaidi
katika mahakama ya wilaya, lakini kutokana na kutokamilika mazungumzo ya
kuwahamishia hapa mkoani, tumekwama kuwafikisha mahakamani. Mazungumzo
yatakapokamilika watarudishwa tena hapa mkoani,” alisema.
Kamanda aliwataka wananchi wawe watulivu katika kipindi
hiki kwani bado uchunguzi unaendelea na mambo haya hayawezi kuisha kienyeji.
Watuhumiwa hao waliokamatwa wakifanya mafunzo ya hayo ni
kiongozi wao, Mohamed Makande (39) mkazi wa Kijiji cha Sengenya, Hassan Omari
(39) mkazi wa Kijiji cha Nalunyu na Rashid Ismail (27).
Wengine ni Abdala Yusufu (32), Salum Bakari (38), Fadhal
Rajabu (20), Abbas Muhidin (32), Ismail Chande (18), Saidi Mawazo (21), Issa
Abed (21) na Ramadhan Issa (26) wote wakazi wa kijiji cha Likokona, wilayani
Nanyumbu.
Kundi hilo la watuhumiwa lilikamatwa na CD 25 zenye
picha za mafunzo mbalimbali yakiwemo ya Al Shabab, mauaji ya Osama Bin Laden,
Zinduka Zanzibar, kuandaa majeshi, mauaji ya Iddi Amini na Mogadishu sniper.
Pamoja na CD hizo pia wanadaiwa kukamatwa na vifaa
vingine ambavyo ni pamoja na DVD player moja solar panel ya watt 30, mapanga,
visu, betri moja ya pikipiki, vitabu mbalimbali vya Kiislamu na tochi.
Pia walikutwa na vifaa vya kupikia na kulia vikiwemo
majiko, taa, baiskeli tatu ndoo za maji, unga wa mahindi kilo 50, mbaazi kilo
50, mfuko wa kijeshi wenye nembo ya nanga ya meli yenye mistari kulia na
kushoto na nyoka katikati.
Kamanda Zelothe alisema kuwa watuhumiwa hao wamefikia 13
baada ya kukamatwa wengine wawili ambao majina yao hakuyataja kwa ajili ya
upelelezi zaidi.
0 comments:
Post a Comment