Watu sitini wamepoteza maisha kutokana na kukanyagana walipokuwa
kwenye hekalu moja katika jimbo la kati la Madhya Pradesh nchini India.
Kwa mujibu wa polisi, tukio hilo limetokea leo kwenye
daraja moja nje ya hekalu la madhehebu ya Kihindu, Wilaya ya Datia, katika
jimbo la Madhya Pradesh.
“Watu sitini wamethibitishwa kupoteza maisha na idadi
inaweza kuongezeka na kufikia 100”, alisema naibu wa Inspekta wa Polisi katika
eneo hilo D.K. Arya.
Kwa mujibu wa Arya, watu walianza kukanyagana baada ya
kuzagaa kwa taarifa kwamba daraja hilo linaweza kuanguka baada ya trekta
kuingia mahali hapo.
“Watu wengi wanahofiwa kuwa waliangukia mtoni na
hawajahesabiwa ili kujua idadi yao.”
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali kutoka eneo la tukio,
zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa.
Maofisa wanasema kuwa watu wapatao 20,000 walikuwa
kwenye daraja hilo wakati wa mkanyagano, huku wengine 400,000 wakielezwa kuwa
walikuwa ndani ya hekalu au jirani na hekalu hilo linalopatikana kaskazini mwa
mji mkuu wa jimbo hilo, Bhopal.
Umati huo ulikuwa umekusanyika kusherehekea na
kuadhimisha sikukuu ya Navaratri.
Mwezi Februari, watu wapatao 40 walipoteza maisha katika
mkanyagano wakati mahujaji wakirejea kutoka kwenye maadhimisho ya kidini ya
sikukuu ya Kumbh Mela jirani na Mto Ganges.
Mwezi Januari 2011, zaidi ya watu 100 walipoteza maisha
yao katika jimbo la Kerala. Mahujaji wengine
224 walifariki mjini Jodhpur mwezi Septemba 2008.
Mara nyingi hutokea matukio ya kukanyagana katika
mikusanyiko mbalimbali ya kidini nchini India, ambayo hupoteza maisha ya watu
na kuwajeruhi wengine.
0 comments:
Post a Comment