Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa
Ummy Mwalimu yupo mkoani Tanga katika ziara ya kikazi, ambapo mwishoni mwa wiki
alizindua mradi wa kuwawezesha wasichana mkoani Tanga chini ya asasi ya TAWEDO kwa
udhamini wa Ubalozi wa Denmark nchini.
Kwa mujibu wa waratibu wa mradi, mpango huo utagusa moja
kwa moja maisha ya wasichana wa mkoa wa
Tanga na kujikita katika kubadilisha fikira
na mitizamo ya wasichana wa jamii ya Tanga na taifa kwa ujumla ili kuweza
kutambua hazina ya wasichana katika kuleta mabadiliko katika jamii zao.
Waratibu hao wamesema kuwa mkazo mkubwa umewekwa kwenye Elimu kwa watoto wa kike, upatikanaji
wa huduma za afya kwa wanafunzi wa kike 1,000 wanaoishi katika mazingira magumu
Tanga. Pia, wasichana walio nje ya shule wa umri wa miaka 12-24 wataunganishwa
katika vikundi vya uzalishaji mali.
Wadau mbalimbali wanaona kuwa hii ni hatua muhimu sana katika
kuchangia maendeleo ya wanawake wa mkoa wa Tanga.
Miongoni mwa waliohudhuria katika uzinduzi wa mradi huo
ni pamoja na Mkuu wa mkoa wa Tanga Mheshimiwa Chiku Galawa, naibu Waziri Ummy
Mwalimu ambae pia ni Mwenyekiti wa TAWEDO, na Mwakilishi wa Balozi wa Denmark Ester Msuya. Wengine ni viongozi mbali mbali,
Wakuu wa wilaya za Pangani, Mkinga na wenyeji Tanga, Mwenyekiti wa UWT mkoa,
mama Aisha Kigoda, na viongozi wengine wa Vyama na Serekali mkoa na Wilaya na wanaafunzi
kutoka Shule za Sekondari na Msingi sambamba na Akina baba na kina mama.
0 comments:
Post a Comment