VIJANA wa Kitanzania 175 wapo katika magereza ya nchini
China kutokana na makosa ya uhalifu yakiwamo ya kusafirisha dawa za kulevya.
Taarifa hiyo ilitolewa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
jana na Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali mstaafu, Abdulrahman
Shimbo, baada ya kiongozi huyo kuwasili nchini humo.
Shimbo alisema kuwa kati ya hao, watatu uraia wao ni wa
kutiliwa shaka. 48 wako China Bara, Hong Kong wapo 117 na Macao wapo 10.
Alisema kuwa wanawake ni 34, ambapo 28 wako Hong Kong na
sita wako China Bara.
Akizungumza na maofisa wa ubalozi pamoja na wajumbe wa
msafara wake, Pinda alisema tatizo la dawa za kulevya linaharibu sifa ya
Tanzania pamoja na mahusiano baina yake na nchi marafiki.
“Tunahitaji kufanya kazi ya ziada ili kupambana na
wasafirishaji wa dawa za kulevya. Watu 175 ni wengi kwa nchi moja lakini cha
kusikitisha zaidi idadi kubwa ni ya wanawake waliokamatwa,” alisema.
Kuhusu misaada ya China kwa Tanzania, alisema kuna
miradi ya kufa na kupona ambayo itabidi iwekewe uzito katika ziara yake hii na
kuiainisha kuwa ni ujenzi wa Reli ya Kati, usambazaji wa umeme na ukuzaji wa
utalii baina ya nchi hizo hasa fursa ya kuanzisha usafiri wa ndege wa moja kwa
moja baina ya China na Tanzania.
Leo Pinda atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi
hiyo, Li Keqiang, Rais wa Benki ya Exim ya China, Rais wa Benki ya Maendeleo ya
China na uongozi wa China Railway Jianchang Engineering. Pia atahudhuria dhifa
ya taifa itakayoandaliwa kwa heshima yake kesho jioni.
Mapema, Balozi Shimbao alimweleza waziri mkuu kuwa
sehemu kubwa ya utekelezaji wa miradi kati ya Tanzania na China iko chini ya
mwamvuli wa FOCAC (Forum on Africa China Co-operation) ambayo inagawanyika
katika maeneo sita.
Pinda aliwasili Beijing, China jana jioni na kuanza
vikao ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa, kwa mwaliko wa
serikali ya nchi hiyo.
0 comments:
Post a Comment