Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa |
Ikiwa yamebaki majuma machache wanafunzi wa kidato cha
nne waanze mtihani wa wa taifa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iko kwenye
mchakato wa kubadilisha mfumo wa upangaji za mitihani ya sekondari na matumizi
wa alama za maendeleo ya mwanafunzi (Continuous Assessment (CA).
Mfumo huo ambao unatarajiwa kuanza kutumika kwenye
Mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka huu, unakuja ikiwa ni miezi michache
tangu Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha kufeli kwa maelfu ya
wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012.
Akizungumzia mchakato huo, Kamishna wa Elimu Profesa
Eustella Bhalalusesa alisema kwamba hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni sehemu ya
kuboresha elimu na kuwa haina uhusiano na taarifa ya tume iliyoundwa na Waziri
Mkuu ambayo mpaka sasa haijawekwa hadharani.
“Mambo yanakwenda yanabadilika hata binadamu yeyote
anabadilika kila siku, mfumo unaotumika sasa hivi ni wa siku nyingi,” alisema.
Alisema kuwa, ili kuweza kuboresha vyema mfumo huo
wameshirikisha wadau mbalimbali zikiwamo shule za sekondari.
“Kama unataka kuboresha lazima upate maoni, lengo letu
ni kushirikisha shule zote za sekondari za Tanzania, ila siwezi kukuhakikishia
kama zote zitashiriki kwa kuwa tunawatumia zaidi maofisa elimu mkoa na wilaya.
Tumeweka pia dodoso kwenye mdandao ili watu zaidi washiriki.
Kuhusu tume ya Pinda hapa haihusiki kabisa, ile ilikuwa
na mambo yake, hata bila ile tume sisi hii tungefanya tu,” alisema Profesa
Bhalalusesa.
Alisema kuwa, mpaka sasa wameshapokea zaidi ya asilimia
60 ya maoni hayo kutokana na lengo walilo jiwekea.
Dodoso hilo ambalo pia Mwananchi imefanikiwa kuliona,
linasema kuwa serikali inakusanya maoni ya wadau wa elimu kuhusu Upangaji wa
Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na
cha sita pamoja na matumizi ya ‘Alama Endelevu ya Mwanafunzi [Continuous
Assessment (CA)].
“Serikali imeamua kukusanya maoni haya kwa sababu kwa
muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika katika mitihani ya
kuhitimu kidato cha nne na kidato cha sita havifanani pamoja na kwamba mitihani
hiyo yote ni ya elimu ya sekondari.
Pia mfumo wa elimu ya sekondari umekuwa na miundo
tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta),” sehemu ya dodoso inasema.
Dodoso hilo linafafanua kuwa, muundo wa kwanza ni ule wa
shule ambao alama mgando (Fixed Grade Ranges) ambao alama zinazotumika kupanga
madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20.
Muundo wa pili ulioidhinishwa kutumiwa na Necta kuanzia
mwaka 2012 ni Upangaji wa Alama Mgando usiobadilika (Fixed Grade Range).
Kwa kidato cha nne alama zilizotumika ni A = 80 – 100, B
= 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49 na F = 0 – 34.
Kwa upande wa kidato cha sita alama zilizotumika ni A =
80 – 100; B = 75 - 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F
= 0 – 39.
Kwa mujibu wa dodoso hilo, alama zinazopendekezwa ni A =
81 – 100, B = 61 – 80, C = 41 – 60, D = 21 – 40 naF = 0 - 20.
Utaratibu
mwingine ambao washiriki wanapaswa kuchagua ni A = 80 – 100, B = 65 – 79, C =
50 – 64, D = 35 – 49 na F = 0 – 34 huku utaratibu wa tatu ukiwa A+ = 91 – 100,
A = 81 – 90, B+ = 71 - 80, B = 61 - 70, C+ = 51 – 60, C = 41 – 50, D+= 31 – 40,
D = 21 – 30, E = 11 – 20 na U = 0 – 10.
Akisoma Kauli ya Serikali Bungeni kuhusu Taarifa ya
Awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha
Nne mwaka 2012, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wiliam Lukuvi alisema
kuwa matokeo yaliyotangazwa awali na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
yafutwe na yapangwe tena kwa kutumia mfumo uliobadilika mwaka 2011 kama
ilivyopendekeza tume ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Hata hivyo, baada ya kufutwa kwa matokeo hayo na
kupangwa upya, Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa utaratibu
uliotumika kupanga matokeo hayo mapya ni uleule uliotumika kuandaa matokeo
yaliyofutwa wa Fixed Grade Ranges.
“Kuanzia sasa matokeo ya mtihani ya kidato cha nne na
sita yatachakatwa kwa kutumia Fixed Grade Ranges na Standardization (alama
zisizobadilika na kuuwisha alama za mitihani),” alisema Kawambwa.
0 comments:
Post a Comment