Bunge la Congress nchini Marekani limepitisha mpango wa
muda mfupi wa kuifungua serikali na kuongeza uwezo wa nchi hiyo wa kukopa.
Muswada wenye kurasa 35, ambao utaongeza uwezo wa nchi
hiyo kukopa mpaka Februari 7 na kufadhili shughuli za serikali mpaka Januari 17,
ulikubaliwa na mabunge yote mawili, bunge la seneti na bunge la wawakilishi,
muda mfupi kabla ya kumalizika kwa muda wa uwezo wa Marekani kukopa fedha na
siku 16 baada ya serikali kufunga shughuli zake.
Bunge la seneti liliupitisha muswada huo kwa kura 81 dhidi
ya 18 na bunge la Wawakilishi liliupitisha mpango huo uliosimamiwa na seneti
kwa kura 285 dhidi ya 144.
Muswada huo umetumwa kwa Rais Obama ambaye ameahidi
kuusaini mara moja pindi utakapowasili mezani kwake.
“Mpango huu utakapowasili mezani kwangu nitausaini mara
moja na tutaifungua serikali mara moja, na tunaweza kuondoa hili wingu la
mashaka na tabu kwenye shughuli zetu na wananchi wa Marekani,” alisema Obama
wakati akisubiri Bunge kupitisha mpango huo.
Kwa kipindi cha siku kumi na sita kuanzia Oktoba 1,
serikali ya Marekani ilisimamisha baadhi ya shughuli zake kwa sababu wabunge wa
Democrat na Republican walishindwa kukubaliana kuhusu bajeti ambayo ingeifanya
serikali iendelee kufanya kazi.
Msuguano mkubwa ulitokana na mpango wa Obama wa huduma
nafuu za bima kwa wananchi wasiokuwa na bima, unaojulikana kama Obamacare, ambao
wabunge wa Republican walitaka uondolewe au ucheleweshwe.
Wasiwasi mkubwa ulizidi kwamba mgogoro huo wa kisiasa
nchini Marekani ungepelekea nchi hiyo kushindwa kuongeza uwezo wake wa kukopa
jambo ambalo lingeifanya Marekani kushindwa kulipa madeni kwa mara kwanza
katika historia ya nchi hiyo.
Spika wa Bunge la Wawakilishi John Boehner (M-Republican
kutoka Ohio) na viongozi wengine wa chama hicho walikubali kushindwa saa chache
baada ya Harry Reid na Mitch McConnell, ambao ni viongozi wabunge wengi na
wabunge wachache katika bunge la Seneti, kutangaza vipengele vya mpango huo wa
muda mfupi.
Hata hivyo, Boehner alisema kuwa wabunge wa Republican
wataendelea na juhudi zao za kumlazimisha Obama kuondosha au kuchelewesha
utekelezaji wa mpango wake wa bima kwa watu wa kipato cha chini.
Habari imeandaliwa na: Mzizima 24
0 comments:
Post a Comment