Wakati Tanzania ikitajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zenye
amani na utulivu, imebainika kuwa Watanzania ni miongoni mwa watu wasio na
furaha na waliokata tamaa hapa duniani.
Ripoti inayoonyesha orodha ya nchi zenye furaha duniani
ya mwaka 2013 (World Happiness Report 2013), imeitaja Tanzania kuwa ni miongoni
mwa nchi 10 za mwisho duniani kati ya nchi 156 zilizofanyiwa utafiti huo.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na kundi la wataalamu kutoka
Umoja wa Mataifa (UN), kati ya mwaka 2010 na 2012, inaonyesha kuwa Tanzania
imeshika nafasi ya 151 ikiburuta mkia pamoja na nchi za Rwanda, Burundi,
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Benin na Togo.
Upatikanaji wa huduma za jamii, mtazamo wa watu kuhusu
rushwa, umri wa kuishi, ukosefu wa kazi, pato la taifa na ukarimu wa watu
katika nchi husika, ni baadhi ya vigezo vilivyoangaliwa wakati wa kuandaa
taarifa hiyo.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alieleza
kushtushwa na ripoti hiyo kwa maelezo kwamba ni asilimia 11.7 tu ya Watanzania
wasio na ajira na kwamba wale wanaofanya kazi, wanapata huduma zote za msingi,
ikiwa ni pamoja na kwenda likizo na mishahara inayolingana na taaluma zao.
“Watanzania wana furaha, kwa upande wa wafanyakazi
wanapata haki zao zote wanazostahili, sijui ni vigezo vipi wametumia…kwa mujibu
wa takwimu za 2006 ni asilimia 11.7 ya Watanzania ndio waliokuwa hawana kazi,
lakini wakati huo idadi ya watu ilikuwa ndogo, hivi sasa imeongezeka,” alisema
Kabaka na kuongeza:“Usafiri ndiyo tatizo linalowasumbua wafanyakazi wengi kwa
kuwa wanachelewa kwenda kazini.”
Naye, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Salum alisema pamoja
na vigezo vingine vilivyotumika kutambua furaha ya Watanzania, umaskini ndiyo
unaoweza kuwa chanzo cha Tanzania kushika nafasi za mwisho.
“Inategemea na vigezo vingine walivyovitumia, nakubali
kuwa Tanzania ni maskini pengine hali hiyo imeifanya nchi kushika nafasi ya
mwisho,” alisema Salum.
Nchi zilizoongoza
Taarifa hiyo imezitaja nchi tano; Denmark, Norway,
Uswisi, Netherlands na Sweden kuwa ndizo zinazoongoza kwa watu wake kuwa na
furaha zaidi duniani, huku Angola ikishika nafasi ya kwanza Afrika na ya 61
duniani ikifuatiwa na Algeria (73), Libya (78), Ghana (86), Zambia (91),
Lesotho (98), Morocco (99) na Swaziland (100).
Kwa upande wa Afrika Mashariki, wananchi wa Uganda ndio
walionekana kuwa na furaha zaidi kwani nchi hiyo imeshika nafasi ya 120
wakifuatiwa na Kenya (123), Tanzania (151), Rwanda (152) na Burundi (153).
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kati ya mwaka 2005 na 2012,
nchi 60 duniani ziliongeza viwango vya furaha kwa watu wake, kati ya hizo 16
zikiwa barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Nchi 29 zilibaki katika viwango vya awali, huku watu
kutoka nchi 41 wakipunguza viwango vyao vya furaha.
Ikilinganishwa na ripoti ilifanywa kati ya 2005 – 2007,
Tanzania imeshuka kutoka asilimia 40 hadi 37. Ripoti hiyo inaeleza kuwa
asilimia 10 ya watu duniani wanasumbuliwa na matatizo ya akili ambayo
yamewasababisha kukosa furaha.
Hata hivyo, imebainika kuwa mtu mmoja anaweza kukosa
furaha kutokana na sababu zaidi ya moja.
“Mtu mmoja anaweza kukosa furaha kutokana na sababu
mbalimbali kama umaskini, ukosefu wa kazi, kuvunjika kwa ndoa na kusumbuliwa na
ugonjwa. Lakini sehemu kubwa, matatizo sugu ya akili yamesababisha kukosekana
kwa furaha,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Alipoulizwa kuhusu ripoti hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema bado hajaiona na kwamba atakapoisoma
atakuwa tayari kuizungumzia.
“Sijaiona ripoti hiyo kwa hivyo siwezi kusema chochote
hadi niione, wewe si umeiona ndiyo maana ukatupa maswali?” alihoji Dk Mwinyi.
Wataalamu wanena
Mwanasaikolojia Modesta Kimonga, alisema Watanzania
wengi wanakuwa na hasira kila wakati kutokana na kukosa matumaini, baada ya
mambo yao kushindwa kufanikiwa.
Alisema hali hiyo inatokana na watu wengi kushindwa
kudhibiti magonjwa na matatizo mengine yanayowakabili.
“Watanzania wengi wanasumbuliwa na mood disorder,
wanakuwa wakali, wenye hasira kila wakati. Mambo yao hayaendi wamekosa tumaini.
Hali hiyo inawakumbwa hata watoto ambao wanakosa mahitaji yao ya msingi,”
alisema Kimonga.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa zipo sababu
mbalimbali zinazowafanya watu kuwa na furaha: “Wanauchumi wanasema furaha
inaletwa na kipato kikubwa, wanasaikolojia wanaamini furaha inakuja baada ya
mtu kuwa na afya njema na viongozi wa dini wanaamini furaha huletwa na maadili
mema,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest
Ngowi alisema kuna uhusiano wa karibu kati ya umaskini na furaha, kwa kuwa mtu
asiye na kipato cha kununua mahitaji yake ya msingi hawezi kuwa na furaha.
“Gharama za bidhaa zipo juu, mtu masikini hawezi kuwa na
furaha, hata hivyo haimaanishi kuwa nchi tajiri ndizo zenye furaha. Nchi kama
Norway pamoja na kuwa na uchumi mzuri, lakini ina idadi kubwa ya watu
wanaojinyonga,” alisema Ngowi.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha
Kijamii, Costantine Akitanda, alisema taarifa hiyo iko sahihi na kwamba karibu
kila Mtanzania analalamika.
“Ukichunguza utagundua kuwa karibu kila Mtanzania
analalamika. Hata sera zilizopo hazina mfumo unaowawezesha watu kunufaika na
maliasili za taifa,” alisema Akitanda.
Pamoja na msukosuko wa uchumi ulioitikisa dunia kuanzia
mwaka 2008, dunia imeshuhudia watu wakiongeza viwango vyao vya furaha kutokana
na sababu mbalimbali kulingana na mahali nchi ilipo.
Mkazi wa Mabibo, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Vick
Manonge, alisema ripoti hiyo inaonyesha hali halisi ilivyo hivi sasa hapa
nchini, kwa kuwa watu wengi wanaonekana kuwa na hasira.
“Kama kuna mtu hakubaliani na hilo (ripoti hiyo)
aangalie kwenye daladala watu walivyo na hasira bila sababu ya msingi, mwingine
hataki aulizwe hata nauli, “ alisema Manonge.
Katika siku za hivi karibuni baadhi ya viongozi wakubwa
duniani wamekuwa wakizitaka Serikali kutunga sera za maendeleo zitakazoendana
na hali halisi ya maisha ya watu wa eneo husika, ili kuweka mazingira
yatakayowaletea wananchi furaha.
Baadhi ya huduma zinazotolewa na serikali ni afya,
kutengeneza ajira, elimu na kuweka mazingira bora ya kujiwezesha kichumi kwa
kila Mtanzania.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment