SHEHENA ya kutisha yenye viungo vya mwili wa binadamu
vilivyoundwa kwa plastiki, ambavyo inashukiwa vilinuiwa kutumiwa katika ibada za
kishetani nchini Kenya ilinaswa Alhamisi katika Bandari ya Mombasa.
Vitu hivyo pia vinahusishwa na watu wenye siri, sherehe
ya kuwakumbuka wafu ama vitu vinavyohitajika katika ukumbi wa michezo ya
kuigiza.
Vitu hivyo ni pamoja na mafuvu ya vichwa, mikono na
miguu, viganja, buibui wakubwa weusi, mawe ya kaburi, maiti na popo.
Afisa wa ngazi za juu wa Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA)
alisema shehena hiyo ni mali ya “mwanasiasa maarufu sana” nchini Kenya .
Vilikuwa vimewekwa katika masanduku 10 makubwa ambayo
hayakuwa na lebo yoyote.
Vitu hivyo vimegunduliwa huku kukiwa na hofu kwamba kuna
vituo vya kuabudu shetani nchini Kenya vinavyoendelea kusajili wafuasi.
Inahofiwa kuwa kama vitu hivyo si vya mchezo wa kuigiza
wa kutisha basi vina uhusiano na ibada za kishetani.
Vilikuwa miongoni mwa mali nyingine iliyosafirishwa
kutoka China lakini havikuwa vimeorodheshwa kuwa sehemu ya bidhaa hizo zingine.
Kamishna Msaidizi wa KRA, Bi Fatuma Yusuf, alisema
uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na shehena hiyo ya kutisha na kwamba aliyekuwa
ameiagiza atatajwa wakati ukifika.
Baadhi ya vitu hivyo vya plastiki vilionyesha jinsi
binadamu anavyoweza kuteseka huku moja ikionyesha mwanamume akilia kwa maumivu
huku akivamiwa na jeshi la panya.
Vingine zinaonyesha miguu ama mikono iliyokatwa huku
ikifuja damu. Pia kuna vibao vilivyoandikwa kwa herufi nyekundu zinazotoka
damu.
THUBUTU
Kimojawapo cha vibao hivyo kimeandikwa “Geuka” na
kingine kimeandikwa “thubutu kuingia.”
Bi Yusuf alisema shehena hiyo, ambayo ilipatikana katika
kituo cha mizigo cha Interpel Container Freight Station, karibu na mzunguko wa
Changamwe, iliwasili Kenya Septemba 3.
“Kontena hiyo ya futi 40 iliwasili kutoka China kama
bidhaa za kawaida za nyumbani. Lakini baada ya kuikagua kwa makini tumegundua
viungo bandia vya mwili wa binadamu yakiwemo mafuvu ya vichwa, mikono na miguu
miongoni mwa vitu vingine,” akasema Bi Yusuf.
Alisema bidhaa nyingine zilizokuwa ndani ya shehena hiyo
na ambazo zilikuwa zimetajwa kuwa ndani ni mashine za kufua nguo, majiko ya
kuoka, pazia, majiko ya gesi, vigae vya sakafuni na ukutani miongoni mwa bidhaa
nyingine.
Bi Yusuf alisema viungo hivyo bandia vya mwili wa
binadamu ndiyo vya kwanza vya aina yake kuletwa Kenya.
Msemaji ambaye hakutaka kutajwa jina alisema vitu hivyo
viliagizwa kutumiwa katika hekalu za siri za kuabudu mashetani katika miji
fulani nchini Kenya.
Alidai kuwa mahekalu hayo yapo Mombasa, Nairobi na
Kisumu.
0 comments:
Post a Comment