ORODHA YA MABILIONEA AFRIKA YATAJWA

Isabel dos Santos one of Africa's richest women. Photo/FILE
Isabel dos Santos mmoja wa wanawake matajiri zaidi Afrika.



JARIDA la Ventures Afrika linaloandika masuala mbalimbali ya uchumi, limetoa orodha ndefu ya mabilionea wa Afrika ambayo imefikia 55 tofauti na ile iliyokuwa ikitajwa awali.

Katika orodha hiyo mpya, mfanyabiashara Mtanzania mwenye asili ya kiasia, Mohammed Dewji, ametajwa kuwa bilionea mdogo kuliko wote sanjari na Igho Sanomi ambaye ni mfanyabiashara wa mafuta na raia wa Nigeria, wote wakiwa na umri wa miaka 38.

Pia katika orodha hiyo wamo wanawake watatu, miongoni mwao ni mama wa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta.

Mama Ngina Kenyatta anaingia katika orodha hiyo, huku familia yake ikitajwa kumiliki vitega uchumi vingi vya biashara ndani na nje ya Kenya.

Mbali na biashara, familia yake inatajwa pia kumiliki eneo kubwa la ardhi linalokadiriwa kufikia robo tatu ya ardhi yote yenye rutuba nchini Kenya.

Kwa mujibu wa tovuti ya Forbes, familia ya Uhuru inamiliki hekta 500,000 za ardhi nchini Kenya.

Pia familia hiyo inamiliki moja kati ya viwanda vikubwa vya maziwa nchini Kenya cha Brookside Dairies, kituo cha televisheni cha K24 na Benki ya Commecial Bank iliyoko jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa jarida hilo la Ventures, mwanaume anayeongoza katika orodha hiyo ni bilionea Aliko Dangote wa Nigeria, mwenye mali zenye thamani ya dola bilioni 20.

Baadhi ya wachambuzi wamesema kuwa huenda orodha hiyo ikazua mjadala, kuhusu pengo lililopo kati ya matajiri na maskini barani Afrika.

Mwezi Aprili, benki ya dunia ilisema kuwa idadi ya watu wanaoishi katika umaskini mkubwa barani Afrika imeongezeka katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, kutoka watu milioni 205 hadi watu milioni 414.

Ripoti iliyotolewa awali na shirika la utafiti la Afrobarometer, ilipendekeza kuwa ukuaji wa kiuchumi barani Afrika unawanufaisha wachache sana.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC, Tomi Oladipo, hii ni mara ya kwanza jarida lenye ushawishi la Ventures la nchini Nigeria, kuchapisha orodha ya Waafrika wenye utajiri mkubwa.

Mabilionea hao 55 waliotajwa na jarida hilo ni wengi zaidi kuliko idadi iliyochapishwa na jarida la masuala ya kifedha la Marekani mwaka jana.

Inaelezwa kuwa sababu ya kugundua matajiri wengi wa Kiafrika, ilitokana na mbinu walizotumia watafiti wa jarida hilo tofauti na zile ambazo zimekuwa zikitumiwa na majarida mengine kufanya utafiti wao.

Kwa mujibu wa jarida hilo, utajiri wa mabilionea hawa ukijumlishwa unakuwa wenye thamani ya dola bilioni 143.88, kila mmoja akiwa na utajiri wa dola bilioni 2.6.

Kati ya mabilionea hawa, 20 ni wa Nigeria, 9 kutoka Afrika Kusini na wanane ni raia wa Misri.

Mwanamke tajiri zaidi ni Folorunsho Alakija wa Nigeria akiwa na mali yenye thamani ya dola bilioni 7.3 kwa sababu ya biashara zake za mafuta. Pia alisomea masomo ya mitindo mjini London na hata kumshonea nguo Maryam Babangida, marehemu mkewe aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa Nigeria, Ibrahim Babangida.

Isabel Dos Santos, muwekezaji wa Angola na mwanawe Rais wa Angola, Jose Eduardo dos Santos, naye pia yumo kwenye orodha hiyo.

Mfanyabiashara wa Afrika Kusini, Allan Gray aliyesomea Chuo Kikuu cha Havard, ndiye tajiri mkubwa nchini Afrika Kusini akiwa na mali zenye thamani ya dola bilioni 8.5.

Nathan Kirsh, kutoka Swaziland anayejishughulisha na biashara za ujenzi, pia yumo kwenye orodha hiyo. Mali yake ni ya thamani ya dola bilioni 3.6 na ana biashara mjini London na New York.

Kwa mujibu wa jarida hilo, idadi hii ya mabilionea huenda ni ndogo kwa sababu Waafrika hawaamini sana kujivunia utajiri wakati unaishi miongoni mwa watu maskini.




Matajiri 10 bora Afrika
1. Aliko Dangote
Dola bilioni 20.2
Sekta: Viwanda
Nchi: Nigeria
Umri: 56

2. Allan Gray
Dola bilioni 8.5
Sekta: Huduma za fedha
Nchi: Afrika Kusini
Umri: 75


3. Mike Adenuga
Dola bilioni 8
Sekta: Mafuta, simu
Nchi: Nigeria
Umri: 60

4. Folorunsho Alakija
Dola bilioni 7.3
Sekta: Mafuta
Nchi: Nigeria
Umri: 62


5. Nicky Oppenheimer
Dola bilioni 6.5
Sekta: Madini, uwekezaji
Nchi: Afrika Kusini
Umri: 68


6. Johann Rupert
Dola bilioni 6.1
Sekta: Bidhaa za anasa
Nchi: Afrika Kusini
Umri: 63


7. Nassef Sawiris
Dola bilioni 5.2
Sekta: Ujenzi
Nchi: Misri
Umri: 53


8. Gilbert Chagoury & Family
Dola bilioni 4.2
Sekta: Ujenzi
Nchi: Nigeria
Umri: 67


9. Nathan Kirsh
Dola bilioni 3.6
Sekta: Nyumba, usambazaji
Nchi: Swaziland
Umri: 82

10. Christoffel Wiese
Dola bilioni 3.4
Sekta: Biashara
Nchi: Afrika Kusini
Umri: 72


CHANZO: Mtanzania
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment