TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Leo, Jumatatu, Oktoba 7, 2013, zimetungwa habari,
zikaingizwa kwenye Mitandao ya Kijamii na kusambazwa sana zikidai kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametia saini
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambao
ulipitishwa na Bunge katika Kikao chake cha mwezi uliopita.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu inapenda
kufafanua kama ifuatavyo:
a) Kwanza, Ofisi ya Rais, Ikulu haijapokea Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Inawezekana Muswada
huo umekwishakutumwa kutoka Bungeni lakini haujamfikia Mheshimiwa Rais. Hivyo,
kama haujamfikia, Mhe. Rais hawezi akawa ameutia saini
b) Pili, Muswada huo ukimfikia Mheshimiwa Rais,
inatarajiwa kuwa atautia saini kwa sababu Muswada huo umepitia katika mchakato
sahihi na halali wa Kikatiba kwa maana ya kufikishwa Bungeni na Serikali,
Kujadiliwa na hatimaye kupitishwa na Bunge.
c) Tatu, kama yapo marekebisho ambayo yanaonekana
yanafaa kufanywa katika Sheria hiyo, basi yatafanywa na Bunge baada ya Mhe.
Rais kuwa ametimiza matakwa ya Kikatiba ya kutia saini Muswada ambao
umepitishwa na Bunge kwa kufuatia mchakato sahihi na halali wa Kikatiba.
d) Nne, na wala hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Sheria
kupitishwa na Bunge, ikatiwa saini na Mhe. Rais na baadaye kufanyiwa
marekebisho na Bunge baada ya kuonekana umuhimu wa kufanya marekebisho hayo.
Mwishoni mwa mwaka 2012, Sheria ya Marekebisho ya Katiba ilipitia njia hiyo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
7 Oktoba, 2013
0 comments:
Post a Comment