JESHI la Polisi visiwani Zanzibar, limesema ndani ya
jamii ya Wazanzibari kuna mgogoro uliojificha unaosababisha kuwepo kwa matukio
yenye sura ya kigaidi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar,
Mkadam Khamis Mkadam, ndiye aliyefichua ukweli huo katika mahojiano yake na
MTANZANIA Jumatano jana kupitia simu yake ya kiganjani.
Kamanda Mkadam ambaye alikuwa akizungumzia uchunguzi wa
awali wa Jeshi la Polisi kuhusu mlipuko wa bomu lililorushwa dukani katika eneo
la Darajani Makontena, alisema taarifa za awali za kikachero zimeonyesha kuwa
upo mgogoro uliojificha miongoni mwa watu wa jamii ya Zanzibar unaosababisha
kuwapo kwa matukio ya kihalifu.
Kamanda huyo alisema, watu waliokuwa katika gari aina ya
Pick Up, walirusha bomu hilo lililokuwa na muundo wa Soseji katika duka la
Sahara Store linalomilikiwa na mfanyabiashara aliyemtaja kwa jina moja la
Himid.
Alisema tukio hilo lilitokea siku ya Jumapili majira ya
saa 8:30 mchana.
Kamanda Mkadam alisema bomu hilo halikuweza kuharibu
duka hilo, badala yake liliangukia sanduku zenye chupa za soda ambapo mmoja wa
walinzi aliyekuwapo eneo hilo, Amour Kassim, alilichukua na kulitupa.
Taarifa za kikachero zimemnukuu mlinzi huyo akieleza
kuwa aliuchukua mfuko uiliorushwa na watu waliokuwa kwenye Pick up, lakini
alibaini kuwa unatoa moshi mwingi ndipo aliurusha barabarani na kutoa kishindo
kikubwa ambacho kilichimba barabara.
Awali Kamanda Mkadam alisema kitu kitakachoweza kusaidia
uchunguzi wa Jeshi la Polisi ni masalia ya unga mweupe na kokoto zilizochimbika
na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati vyombo vya usalama vikiendelea
kufanya uchunguzi.
Kamanda Mkadam alisema taarifa za awali za polisi
zimeonyesha yapo makundi ya watu Zanzibar walioamua kutendeana visa, ikiwa ni
pamoja na tukio la kurushwa bomu eneo la darajani eneo la maduka, pamoja na
matukio ya watu kushambuliwa kwa tindikali.
“Tunatafuta taarifa za makundi yanayofanyishiana, upo
mgogoro mkubwa kati ya watu na watu au makundi kwa makundi, hizi ni taarifa za
awali za kipolisi kwamba kuna mgogoro umejificha.
“Kuna uhalifu uliojificha na tumeanza kupata taarifa
zake na tutawaeleza hivi karibuni, kwa sasa ni mapema mno kuueleza umma,”
alisema Mkadam.
Kamanda Mkadam alisema polisi inaendelea kufanya kazi
yake ya upelelezi kwa uhakika juu ya tukio la kurushwa bomu la mkono na yale ya
watu kushambuliwa kwa tindikali, ili wasipotoshe ushahidi.
“Tumehoji watu wengi na bado hatujakamata, tunafanya
kazi yetu kwa uhakika ili tuwe karibu na taarifa zetu, tunajitahidi kutafuta
habari,” alisema.
CHANZO: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment