WATU Sita, wakiwemo raia wawili, wamepoteza maisha na
wengine kadhaa kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu uliotokea jirani na kambi moja
ya jeshi kaskazini mwa Mali.
Tukio hilo lilitokea jana Jumamosi baada ya gari
lililokuwa na mabomu kulipuka katika mji wa Timbuktu ulio kaskazini mwa nchi
hiyo.
Ripoti zinasema kuwa askari sita wa jeshi la nchi hiyo
ni miongoni mwa walioathiriwa na mlipuko huo, huku nyumba kadhaa zikiharibiwa
kabisa.
Serikali ya Mali imelaani vikali shambulizi hilo, ambalo
limetekelezwa siku kadhaa baada ya wapiganaji wa Tuareg wanaopigania kujitenga
kwa eneo la kaskazini kusitisha mazungumzo na serikali, wakiituhumu kwa
kushindwa kutekekeleza ahadi zake kuhusu makubaliano ya amani.
Mwezi Juni viongozi wa Kituareg na viongozi wa mpito wa
serikali ya Mali walifikia makubaliano ya kuliruhusu jeshi kurudi katika eneo
la Kidal na kufanyika kwa uchaguzi wa urais.
Tukio la jana ni la pili kufanywa dhidi ya vikosi vya
jeshi tangu Septemba 26.
Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita, amelifanya suala
la maridhiano kuwa kipaumbele chake cha juu cha utawala wake tangu aliposhinda
uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment