Askari wa Kenya wakijiandaa kukabiliana na wavamizi katika kituo cha biashara cha Westgate, Nairobi, tarehe 23/9/2013 |
MAAFISA wawili wa Polisi nchini Kenya wameuawa katika
shambulizi lililotekelezwa dhidi ya kituo kimoja cha polisi katika mji wa kasikazini
wa Mandera, mpakani mwa Somalia.
Kamanda wa polisi katika eneo hilo, Charlton Mureithi,
anasema kuwa watu watatu pia walijeruhiwa katika shambulizi hilo lililotokea
leo asubuhi, huku magari kumi yakiteketea kwa moto.
Mashuhuda wanasema kuwa watu wenye silaha
walikishambulia kituo hicho kwa mabomu ya kurushwa kwa mkono kisha wakakimbia
na kukiacha kituo hicho kikiwaka moto.
“Hakuna aliyekamatwa mpaka sasa. Wamesababisha uharibifu
mkubwa,” alisema Mureithi.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo,
ambalo limetokea siku moja baada ya raia mmoja kuuawa na wengine wanne
kujeruhiwa katika shambulizi kama hilo katika mji wa kaskazini mashariki wa
Wajir.
Mashambulizi hayo yametokea siku chache baada ya kundi
la al-Shabab kukivamia kituo kimoja cha biashara mjini Nairobi na kuua watu 70
huku sehemu ya jengo hilo ikiharibiwa vibaya sana.
Jana Jumatano, kiongozi wa al-Shabaab, Ahmed Godane,
alithibitisha kuwa kundi lake lilihusika na shambulizi la Nairobi, kwa madai
kuwa walifanya hivyo katika kulipa kisasi cha uvamizi wa jeshi la Kenya kusini
mwa Somalia mwezi Oktoba 2011.
“Ondoeni majeshi yenu, la sivyo jiandaeni kwa vita ya
muda mrefu, umwagaji damu, uharibifu na kuwahamisha kwa nguvu,” alisema Godane katika ujumbe wa sauti
uliowekwa kwenye tovuti moja inayohusishwa na al-Shabab.
Kenya ina zaidi ya askari 4,000 kusini mwa Somalia,
ambapo imekuwa ikipambana na al-Shabaab tangu mwaka 2011.
Askari wa Kenya ni sehemu ya Kikosi cha Umoja wa Afrika
kwa ajili ya Somalia (AMISOM).
0 comments:
Post a Comment