Mlipuko Arusha, CUF Yatoa Tamko

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE 8/05/2013
YAH: MLIPUKO WA BOMU ARUSHA NA MUSTAKABALI WA NCHI YETU


Siku ya Jumapili tarehe 5 mwezi 5, 2013 kulitokea tukio baya na la kikatili dhidi ya uhai Watanzania wenzetu na mustakabali wa amani na utulivu wa nchi yetu kwa ujumla. Mlipuko wa bomu lililorushwa katika kanisa la Mtakatifu Josefu Mfanyakazi huko Olasiti Arusha wakati waumini wa kanisa hilo wakiendelea kuabudu uliua watu wapatao wawili na kujeruhi vibaya wengine zaidi ya 70.
CUF chama cha Wananchi tumeshtusha, kusikitishwa na kukasirishwa sana na tukio hili ambalo lina nia mbaya ya kuchochea moto wa hisia za udini miongoni mwa Watanzania.
CUF tunatoa pole za dhati kwa waathirika wote wa tukio hili waliopotelewa na ndugu zao na wote waliojeruhiwa Mwenyezi Mungu awasaidie wapone haraka waweze kuendelea na shughuli zao za kujenga maisha.Tunatoa pole nyingi kwa Kanisa Katoliki nchini hasa kwa Askofu Lebulu wa Arusha na Balozi wa Papa nchini Tanzania Askofu Fransisco Padila kwa msukosuko walioupata wakati wa mlipuko huo.
Siku ya jumapili mimi nilikuwa Mwanza nikiendelea na harakati za kuelimisha na kujifunza toka kwa Umma wa Watanzania kuhusu Agenda ya Maendeleo kwa Wote (Agenda for Inclusive Development). Katika Mkutano wa hadhara tulioufanya Mjini Mwanza nililaani vikali tukio hili la kinyama na kuwapa pole wafiwa na waliojeruhiwa, waumini na viongozi wa Kanisa Katoliki waliohudhuria misa katika kanisa la Mtakatifu Josefu Mfanyakazi. Waliohudhuria mkutano wetu walisimama kimya kwa dakika moja kuwaombea waliofariki, na kumuomba Mungu awasaidie kupona haraka waliojeruhiwa.


Baada ya kupata taarifa ya kitendo hiki kiovu, Viongozi wa CUF tulishauriana na kukubaliana kuwa Katibu Mkuu wa Chama chetu Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Singida kwa ziara asitishe shughuli na aende Arusha kuwapa pole na kuwafariji wafiwa, majeruhi, waumini na viongozi wa Kanisa Katoliki. Tarehe 7 Mei, Maalim Seif alienda katika kanisa la Mtakatifu Josefu Mfanyakazi kuona eneo lililorushiwa bomu, alionana na kuwapa pole Baba Askofu, Josephat Lebulu - Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, na Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla.Maalim pia alienda kuwapa pole majeruhi katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru. Kabla ya kuondoka Uwanja Ndege wa Arusha, Maalim Seif alikutana na Rais Jakaya Kikwete ambaye alikuwa karejea nchini baada ya kusitisha ziara yake ya Kuwait kuja kuwapa pole wahanga wa tukio hili na kuongoza na kusimamia juhudi za polisi na serikali kwa ujumla kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wote waliohusika na mauaji na kitendo hiki cha kinyama.

Tukio hili ni mfulilizo wa visa mbalilimbali vilivyopita hapo awali vinavyoendelea kubeba hisia za udini. Mfano ni kushambuliwa kwa nyumba za ibada na kushambuliwa viongozi wa dini.
Kwa muda sasa matukio kama haya yamekuwa yakiendelea kutokea hapa nchini na watekelezaji wa matukio haya kutopatikana. Kitu kibaya ni kwamba wanaopanga mikakati na kunufaika na matukio haya wamekuwa hawajulikani na nia yao kutowekwa wazi.
CUF chama cha wanachi kinaitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina na kuwa wazi katika kutoa taarifa kwa wananchi ambao wanataka kujua lengo na nia ya wapangaji na waandaji wa matukio haya. Serikali itoe maelezo yanayojitosheleza kuhusu hatua madhubuti zinazoenesha kubaini chanzo cha tatizo na suluhisho la muda mrefu.
Ni muhimu vyombo vyetu vya usalama kuwa wazi na uchunguzi unapokamilika taarifa ziwekwe wazi ili umma uweze kujua nini kinaendelea na vyombo vya habari viruhusiwe kuwahoji watoa taarifa. Hii itasaidia kufuta mwanya wa Wananchi kujenga hisia za kushutumiana wao kwa wao ama kuogopana kwa hisia ambazo zinajengwa na matukio yanayoibua maswali yasiyojibika na kuwagawa watanzania ilihali serikali ina majibu ya maswali hayo.
Mfano kwa matukio ya kushambulia nyumba za ibada na viongozi wa dini wapo wanohisi kwamba ni ugaidi, wapo waohisi kwamba ni chuki za kidini, wapowanaohisi kwamba ni siasa za kufanya nchi isitawalike, wapo wanohisi kwamba ni msukumo wa nchi za nje ili kukwapua utajiri wetu n.k. Mpaka hivi sasa serikali haijatoa jibu sahihi. Serikali inawajibika kuwaeleza wamiliki wa nchi yaani Wananchi nini kinaendelea nchini.
CUF tuanaamini kwa serikali makini, imara na iliyoapa kutetea katiba ya nchi hasa kuwalindi Wananchi inauwezo mkubwa wa kudhibiti haya yanayotokea hivi sasa hapa nchini. Ni wajibu wa serikali kufanya hivyo ili wananchi wasipoteze kabisa imani dhidi ya serikali iliyoko madarakani.
Mwisho CUF tuanatoa wito kwa Watanzania wote tusikubali matukio haya kutugawa bali tubaki kuwa imara na wamoja katika kuijenga nchi yenye maendeleo na amani. Kila Mtanzania lazima akumbuke kubeba jukumu la kulinda amani na usalama wa nchi kwani madhara ya kuondoka usalama wa nchi hayachagui mtu, jamii wala mahali. Sote tutaumia. 


CUF tunapongeza kauli ya Baba Askofu Muadhama Kadinali Polycap Pengo kwamba suala zima la tukio la Arusha halihusiani na imani yoyote ya kidini kufuatana na taarifa alizofikishiwa na watu anaowaamini kuwa hawawezi kumdanganya. Zaidi ya hapo ameeleza “Lengo la msingi kabisa, langu na la kanisa ni kwamba tukio lolote lile liwe kwa nia mbaya au nzuri kwa upande wetu isiwe ni sababu ya kuanza mapambano na kuwa chimbuko la ukosefu wa amani katika nchi yetu,”
Watanzania tuna historia, silka, na utamaduni wa kuheshimiana katika imani zetu. Tusikubali kata kata vitendo vya kikatili vya watu wachache sana kupandikiza mbegu ya uhasama baina ya waumini wa dini tofauti. Katika kipindi hiki kigumu kila Mtanzania awe makini katika kujenga mahusiano mema, udugu na urafiki na kila Mtanzania mwenzake. Viongozi wetu wa dini wa madhehebu yote wafanye juhudi ya kubadilishana mawazo kuhusu kuendeleza amani na maelewano baina ya waumini wa dini zote. Viongozi wa dini na wanasiasa tuwe makini katika kauli zetu zisimwagie petroli katika moto wa udini tunaopaswa kuuzimisha kwa kuwatendea haki sawa wananchi wote.
Imetolewa na
Mwenyekiti wa CUF taifa,

Prof.Ibrahimu Lipumba.


Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment