WABUNGE WA CCM WAVUANA NGUO

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda


WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana waliumbuana na kushutumiana wazi mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Hatua hiyo ilifikiwa katika kikao chao katika ukumbi wa Msekwa mjini hapa ambako waliumbuana na kushutumiana waziwazi.
Kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kilifanyika baada Spika wa Bunge, Anne Makinda kuahirisha mjadala wa makadirio ya mtumizi ya fedha ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Spika aliahirisha mjadala wa makadirio hiyo uliokuwa uhitimishwe jana, baada ya wabunge wengi kuonyesha nia ya kuyakwamisha kutokana na kutoridhishwa na jitihada za Serikali za kukabiliana na kero ya maji nchini.

Chanzo chetu kilichokuwa katika kikao hicho kilisema mjadala ulipoanza, Pinda aliizungumzia kwa kifupi Wizara ya Maji na kuonyesha jinsi Serikali ilivyokubali kwa dhati kurekebisha makadirio ya matumizi ya fedha ya wizara hiyo.

Baada ya hoja hiyo, chanzo hicho kilisema Waziri Mkuu aliwasilisha hoja nyingine iliyowataka wabunge wa CCM kuchangia posho zao za siku moja kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

“Hoja hiyo ilipopita, Nyoka wa Shaba (Kangi Lugora, Mbunge wa Mwibara), alisimama na kuhoji ni kwa nini chama kimekubali kusaidia uchaguzi wa madiwani wakati huwa hakisaidii kesi za uchaguzi za wabunge.

“Si unajua Nyoka wa Shaba naye ana kesi mahakamani, sasa ndiyo maana akaamua kuhoji iweje yeye hasaidiwi na chama wakati huo huo anaambiwa asaidie uchaguzi wa madiwani.

“Alipomaliza kusema hivyo, akasimama Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba. Aliposimama aliwashutumu moja kwa moja Lugora na Filikunjombe (Deo, Mbunge wa Ludewa).

“Akasema wabunge hao badala ya kuisaidia Serikali wanapokuwa bungeni, wao wamekuwa wakiishambulia jambo ambalo halileti picha nzuri kwa wananchi.

“Akasema kitendo cha Filikunjombe kusema bungeni kwamba Serikali ina miwani ya mbao hakikuwa kizuri… akasema ‘hawa wenzetu hatuko nao na kwa kuwa mwezi ujao tutaonana na Mwenyekiti wa Chama (Rais Jakaya Kikwete) nitasema mengi’.

“Alipomaliza kusema hayo akasimama Kibajaji (Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera). Kibajaji akaungana na Nkumba, akawashambulia Lugora na Filikunjombe kwamba wanaiua Serikali kutokana na maneno yao bungeni.

“Akasema kama Lugora ana kesi mahakamani ni bora akakabiliana nayo mwenyewe kwa sababu inaonekana hayuko pamoja na chama,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Baadaye alisimama Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima ambaye alimshutumu Lugora kwamba kitendo chake cha kuliambia Bunge kuwa kuna baadhi ya mawaziri wanajihusisha na dawa za kulevya, kinawaweka njia panda wananchi kwa kuwa wanahisi wabunge wao ambao ni mawaziri, nao wamo kwenye orodha hiyo ikizingatiwa kuwa hakuwataja majina.

“Pia, akahoji kama wabunge wana kero zao ni kwa nini wasiwafuate mawaziri na kuzungumza nao badala ya kuwasema bungeni.

“Kisha, alisimama Mangungu (Mbunge wa Kilwa Kaskazini) ambaye alionyesha wasiwasi juu ya majaji wanaosikiliza kesi za uchaguzi.

“Yeye akasema kesi nyingi za uchaguzi ambazo CCM inashindwa ni kwa sababu majaji wengi wanaichukia CCM na wanaipenda Chadema.

“Baadaye aliungwa mkono na Dk. Chami (Dk. Cyril Chami, Mbunge wa Moshi Vijijini) ambaye alidiriki kumtaja jaji mmoja kwa jina kwamba ana upendeleo wa wazi wazi kwa Chadema.

“Kisha, alisimama Mbunge wa Karagwe (Gosbert Blandes) na akatoa ushauri kwamba kuna haja chama kusaidia majimbo ya uchaguzi na wakati huo huo, viongozi wakuu wa chama waende kwa wananchi kama wanavyofanya viongozi wa Chadema.”

Mbali na hao, chanzo hicho kilimtaja Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia kwamba alimshutumu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kwamba hakusaidia wakati wa vurugu zilizotokea hivi karibuni mjini Mtwara.

“Ghasia alianza kwa kusema kwamba, siku hizi Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, anafanya ziara za mara kwa mara jimboni kwake Mtwara Vijijini lakini CCM haijali.

“Pia akamlalamikia Waziri Nchimbi kwamba wakati wa vurugu za wananchi mkoani Mtwara alimpigia simu lakini hakupokea na hata alipomtumia ujumbe mfupi wa simu hakumjibu.

“Akahoji pia kwamba iweje wakati wa vurugu zote Mtwara, nyumba zinazochomwa ni za wabunge wa CCM wanawake na nyumba za wabunge wanaume hazichomwi, akahoji kuna kitu gani hapo,” kilisema chanzo hicho.

FILIKUNJOMBE AJIBU MAPIGO

Wakati mjadala huo ukishika kasi, chanzo hicho kilisema, wakati wote Filikunjombe na Lugora walikuwa wakitaka kujieleza, lakini mara zote Waziri Mkuu ambaye alikuwa kiongozi wa kikao alikuwa hawapi nafasi.

Kutokana na hali hiyo, Filikunjombe alipoona Waziri Mkuu anakaribia kuhitimisha kikao akaamua kusimama na kusema anataka kutoa taarifa.

“Alipopewa nafasi akawashambulia mawaziri kwa kusema kwamba baadhi yao siyo wachapa kazi na akamtolea mfano Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe.

“Akasema Profesa Maghembe anafanya kazi chini ya kiwango na kwamba hata katika wizara zote alizopita hakuwahi kufanikiwa ingawa amekuwa akihamishwa wizara mbalimbali.

“Akasema kwamba CCM inatakiwa iwe na miradi ya uhakika kama kilivyo chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC ambacho kina miradi ya uhakika inayowafanya watu wapende kufanya kazi ndani ya chama hicho kuliko ilivyo kwa CCM.

“Akasema anamshangaa Nkumba kumshambulia yeye na badala yake mashambulizi hayo hayapeleki kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye ndiye amekuwa akitoa baadhi ya maelekezo.

“Yaani katika maelezo yake akasema kitendo chake cha kuikosoa Serikali kiko sahihi kwa sababu haridhishwi na mwenendo wa baadhi ya watendaji,” kilisema chanzo chetu.

KANGI LUGOLA 

Mbunge huyo alipopewa nafasi kwa mujibu wa chanzo chetu, alitishia kuwataja majina mawaziri wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

“Kabla ya hapo, alisema baadhi ya wabunge wa CCM ni wanafiki kwa sababu wanajifanya wanakipenda chama wakati hawakipendi.

“Akasema kama Serikali haifanyi kazi kwa nini asiikosoe, akasisitiza kwamba hatanyamaza na hatasita kuikosoa Serikali kama itaendelea kufanya makosa na akamtaja Nkumba kwamba aache unafiki.

“Baadaye akamgeukia Malima, akamwambia kama anamuona yeye hakufanya vizuri kusema kuna baadhi ya mawaziri wanajihusisha na dawa za kulevya na akashindwa kuwataja majina, kwa nini Rais Kikwete aliposema anawajua wauza dawa za kulevya hakumtaka awataje kwa majina?

“Kangi akawa mbogo akasema ‘kama unafikiri siwajui, sasa ngoja niwataje’. Aliposema hivyo ukumbi mzima ukalipuka na kusema, ‘usiwataje’, ‘usiwataje’,” kilisema chanzo hicho.

“Pia akawaambia mawaziri kwamba wao hawapatikani kwa urahisi na kwamba ni rahisi kuonana na Rais wa Marekani, Barack Obama au Rais mstaafu wa nchi hiyo, George Bush kuliko kuonana na mawaziri wa Tanzania,” kilisema chanzo hicho.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, mwingine aliyezungumza katika kikao hicho ni Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina ambaye alimshambulia Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya kwamba hakustahili kumbeza juzi alipokuwa akijibu hoja yake iliyohusu deni la taifa.

“Mpina akasema ingawa Saada alimjibu kwa kumdhalilisha alitakiwa aone CV (wasifu) yake (Mpina) kwanza kwa sababu anajua mambo mengi kuliko anavyofikiria.

“Mwingine aliyezungumza ni Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo. Huyu aliwaunga mkono wabunge wanaoikosoa Serikali kwa kusema kwamba wako sahihi na kwamba yeye kwa sasa hafanyi kazi hiyo kwa kuwa ameshazeeka,” kilisema chanzo hicho.
CHANZO: Mtanzania
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment