TUKIMWONA SELASINI JASIRI, CHAMA KITAKUFA

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema)



Nimemsikiliza Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) na nahau zake bungeni, nimevutiwa na kauli aliyoitoa kwamba, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuna udini.

Katika matamshi yake anasema, CD alizokuwa nazo zinaonesha namna UDOM kinavyoendeshwa kidini na kwamba kuna wahadhiri ambao wamekuwa wakiwakusanya wanafunzi na kuwapandikiza chuki dhidi ya dini nyingine.

Amenukuliwa kwamba, baada ya wanafunzi hao kulishwa maneno ya chuki na wahadhiri hao wa dini fulani, wakahoji huko nyumbani tunakaa na wanafunzi wa vyuo vingine, tuwafanyeje?

Haya si maneno mepesi kama anavyodhani kwa kuwa, kama tumefikia hali hiyo basi tupo mashakani. Ni maneno yanayohitaji utafiti wa kina ili kujiridhisha ingawa yeye mwenyewe anatilia shaka kauli yake.

Makamu wa UDOM ni Prof. Idrisa Kikula ambaye kwa lugha nyepesi tunaweza kusema kwamba, ndiye Mtendaji Mkuu wa UDOM.

Selasini anasema, UDOM kuna udini na anashangaa sababu za polisi kushindwa kuchukua hatua, yeye hakwenda kutoa taarifa polisi, hajapeleka ushahidi wake polisi na wala hakushughulishwa na walinzi wa amani nje ya bunge, amewapuuza.

Amekimbilia bungeni na CD zake akiamini ataonekana ‘live’ na ujumbe wake utafika kwa aliyemkusudia na kuwaridhisha wale walio nyuma ya mchezo huo, kweli tumemuona na ujumbe wake umefika.


Pengine angeenda polisi huenda lile alililokusudia ama dhamira ya wale walio nyuma yake lisingekuwa na matokeo chanya kama alivyokusudia ama walivyokusudia jamaa zake.

Amefanikiwa kumwaga machache yaliyo kwenye ulimi wake na kuhifadhi mengi moyoni mwake. Huyu ni Selasini nadni ya Chadema.

Waliomwelewa vizuri Selasini huenda wakawa na mtazamo kama wangu kwamba, tafsiri yake isiyo sahihi ni kuwa, Mtendaji Mkuu wa UDOM ni mdini ka kwa hivyo anaendesha chuo kidini na kwa kuwa ni Muislamu, maana yake anaendesha chuo Kiislamu. Pengine Selasini aliona ugumu kutaja Uislamu lakini hakuna tafsiri tofauti na hiyo.

Kwa mantiki hiyo, kilio cha Selasini na wale walio nyuma ya mchezo huo ni kutaka Prof. Idrisa awekwe kando kwa kuwa, anaendesha chuo hicho Kiislamu.

Pia kwa tafsiri ni kwamba, Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) kinachoongozwa na Makamu Mkuu wake Gerald Monela kipo salama. Hakina shaka kwa upande wake maana hajakituhumu.

Chuo Kikuu cha Mzumbe kilicho chini ya Makamu Mwenyekiti wake Joseph Kuzilwa kipo salama na hakuna tuhuma zozote za udini.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinachoongozwa na Prof. Mukandara nacho kimeepuka tuhuma za udini sawia na vyuo vyote vya serikali.

Kwa sasa, kwa bahati mbaya, tuhuma za udini zipo kila sehemu yenye mikusanyiko ya watu wenye dini tofauti, zipo katika kila chuo, zipo sekondari kama ilivyotokea kwenye sekondari ya Bagamoyo na pia zipo Shule za Msingi.

Karibu vyuo vyote vya serikali mambo haya yanalalamikiwa lakini kunyooshea chuo kimoja, hapa ndio Selasini alipoleta tafsiri mbaya kwa jamii.

Selasini anakosea kitu kimoja, ni dharau kwamba, Watanzania hawawezi kutambua kilicho nyuma ya mpango wake na wale waliomtuma. Anajivika bomu la kutugawa, tena ndani ya muhimili wa dola: Bunge.

Lakini pia anaanzisha vita ambayo itammaliza yeye mwenyewe pamoja na chama chake, vita ambayo mwenyekiti wake Freeman Mbowe amekuwa akipambana nayo kwa muda mrefu sasa, anajitahidi kubadilisha fikra za wale wanaoitazama Chadema kwa mtazamo hasi wa kidini.

Mbowe anatambua kwamba, wapo wanaoitafsiri Chadema kwa mtazamo ‘usio sahihi’. Anapambana na mtazamo huo kwenye najukwaa na kwenye vikao vidogo lakini anaangushwa na watu kama akina Selasini.

Chadema inateswa na mambo makuu manne kwa sasa ikiwa ni pamoja na udini, ukanda, urafiki na mashambulizi kutoka vyama vingine.

Inakabiliwa na mtihani mzito kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilicho na vijana wake wengi ndani ya chama hicho, kinakabiliwa na Chama cha Wananchi (CUF) kutaka kurudi katika nafasi yake hiyo, kinakabiliwa na changamoto kutoka NCCR-Mageuzi, lakini yote haya yanapuuzwa na Selasini.

Selasini huenda alionesha hayo nje ya bunge na kuona haitoshi, ameamua kusimama sehemu takatifu na kuwahakikishia walio tofauti na yeye kwamba, yeye ama chama chake kinaendesha mapambano dhidi ya watu wasio na imani yake.

Selasini anadhihirisha chuki yake ana ya chama chake dhidi ya watu walio tofauti na imani yake, Selasini anahitaji kusifiwa ama kuitwa jasiri kwa kuwa, pale wenzake wanapoficha kauli zinazoashiria mpasuko, yeye anajipiga kifua na kutoka hadharani.

Kama chama chake kitaendelea kukaa kimya kutokana na kauli zake zenye kuashiria mapasuko wa kidini, Selasini anaweza kutafsirika kuwa mawazo yake ndio ya chama chake.

Wakati mwingine ni dhambi kusema imani yake ndio chama chake lakini kwa jinsi wanavyopokezana kijiti na wenzake, napata shida kutoamini hivyo.

Selasini anakivuruga chama kwa kukataa kuwa tayari kwa lolote pale alipotakiwa kusaini kwamba, CD zile ni yeye aliyezikabidhi kwa katibu wa Bunge. Bunge limeshindwa kupokea CD zake kutokana na yeye kutokuwa tayari kwa matokeo yoyote pale uchunguzi na upembuzi yakinifu utakapofanywa kutokana na CD hizo.

Naweza kutafsiri kwamba, Selasini alikuwa na malengo yake hasi ya kuvuruga Watanzania wanaohaha katika vikao mbalimbali kuhakikisha wanatuliza upepo wa shetani unaovuma kwa sasa.

Kwa bahati mbaya, Selasini ni Mbunge, anasahau kwamba hata walio na imani tofauti na yeye walimchagua kuwa mbunge, anataka kuwadhiahaki kwamba, ni wapuuzi wasiojua walilolifanya.

Sina hakika kama Selasini atagombea tena na kupata kura ya wale anaowadharau, anaowaona hawana hadhi ya kuwa viongozi wa taasisi kubwa, anaowatuhumu pasina ushahidi wa kweli tena mbele ya Watanzania.

Selasini anapaswa kukumbushwa kwamba, kauli zake na mifano yake anayotaka kuithibitishia jamii inamtesa Mbowe pamoja na Chama chake ambacho mpaka sasa hisia za baadhi ya watu ni hasi hasa kwa upande wa dini.

Kauli zake sawia na za rafiki zake, Godbless Lema, Peter Msigwa, Wenje zitaitesa Chadema mbele ya safari, zinazidi kutia gazi kwa wale waliokuwa na taswira hasi dhidi ya chama hicho. Bila shaka matokeo yake ni mwaka 2015.
Tusubiri.
CHANZO: FAHAMU

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment