Mauaji gerezani: Mfungwa apigwa hadi kufa ndani ya ofisi ya Mkuu wa Gereza

Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali John Minja



UONGOZI wa Gereza la Kisongo mkoani Arusha unatuhumiwa kuwapiga na kuwatesa wafungwa na mahabusu, kiasi cha kusababisha kifo cha mfungwa mmoja na kuwapo majeruhi kadhaa.

Vyanzo vya habari kutoka gerezani hapo vimemtaja mfungwa aliyeuawa kutokana na kipigo kutoka kwa maofisa wa magereza kuwa ni Wilfred Mallya, mfungwa namba 315 ya mwaka 2003, aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha jela.

Taarifa zimesema kuwa mfungwa huyo alipata kipigo kikali ofisini kwa Mkuu wa Gereza hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) L.W Msomba, Januari 24, na kufariki dunia kesho yake, Januari 25 mwaka huu na baadaye mwili wake ulihifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alikiri kupata taarifa za tukio hilo la kusikitisha, na kusema iliundwa timu kuchunguza.

Uchunguzi wa Rai umebaini kuwa timu iliyoundwa na Jeshi la Magereza kuchunguza tukio hilo, ilikuwa chini ya Ofisa Mwandamizi wa jeshi hilo aliyefahamika kwa jina la Juma Malewa.

“Ni kweli taarifa za tukio hilo zilifika ofisini kwangu miezi michache iliyopita, lakini kuna timu ilienda kuchunguza, ninashauri uwasiliane na Kamishna Jenerali wa Magereza, naamini atakuwa na majibu sahihi.

“Pia unajua Mkuu wa Gereza la Kisongo ni mgeni kiasi pale, na wafungwa wanamchukia kwa sababu amedhibiti uingiaji wa bangi na sigara gerezani,” alisema Dk. Nchimbi.

Alipogiwa simu jana, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Minja, alisema yupo nchini Zambia, kwa hiyo asingeweza kuzungumzia suala hilo pamoja na kulifahamu vizuri, na akasema atafutwe Msemaji wa Jeshi hilo, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Omary Mtiga.

Kamishna Jenerali Minja anatajwa kutembelea gereza hilo Desemba 23, 2012, ambapo alielezwa kuhusu vitendo vya unyanyasaji wa wafungwa, na kupewa mfano wa mfungwa aliyevunjwa mguu kutokana na kipigo cha askari.

Msemaji wa Jeshi la Magereza hakuweza kupatikana jana, kutokana na simu yake ya mkononi namba 0784 310 178, kuita bila kupokewa, na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakujibu.

Chanzo cha tukio:

Kwa mujibu wa chanzo chetu, tukio la kupigwa na baadae kufariki kwa Mallya lilitokana na kutajwa na mfungwa mwenzake anayedaiwa kujihusisha na vitendo vya ushoga gerezani, kuwa marehemu alikuwa mmoja wa ‘mabwana’ zake.

Mfungwa huyo ajulikanaye kwa jina la Galinoma Lazaro mwenye namba 13 ya mwaka 2012 anayetumikia kifungo cha miaka 5, anadaiwa kukutwa na askari Magereza akilawitiwa na mwenzake, ambapo alipelekwa hospitali, na ikathibitika baada ya kupimwa kuwa alifanya kitendo, ambacho ni kinyume cha sheria.

Baada ya tukio hilo, askari walimhoji mfungwa huyo ambaye anadhaniwa kuwa na matatizo ya akili, na kumtaka awataje ‘mabwana’ zake wengine, ambapo alimtaja Mallya.

Taarifa zinasema kuwa, Mallya alipoitwa ofisini kwa Mkuu wa Gereza mbele ya maofisa usalama wawili, Inspekta Victor Ngwale na Inspekta Wilson Mshida, na kuulizwa, alionekana kuchukizwa na tuhuma hizo dhidi yake.

Marehemu ambaye kutokana na tabia njema pamoja na kukubali na kuheshimu sheria na taratibu za gerezani, alipewa cheo cha unyapara, baada ya kuchukizwa na tuhuma dhidi yake, aliamua kuvua mkanda wanaovaa wanyapara na kuutupa, kitendo kilichomuudhi Mkuu wa Gereza na kuamuru apewe adhabu ya kupigwa virungu na maaskari.

Taarifa zimesema kuwa, baada ya kipigo hicho alipelekwa kwenye chumba cha adhabu bila kupewa matibabu stahiki, ambapo siku iliyofuata hali yake ilizidi kuwa mbaya, na kufariki dunia.

Pia Rai imefanikiwa kupata majina ya wafungwa waliopigwa siku chache zilizopita na kuumizwa vibaya kuwa ni pamoja na Chrispin Otieno mwenye namba 29 ya mwaka 2012, Ally Ramadhani mwenye namba 452 ya mwaka 2012 na Joseph Sironga mwenye namba 395 ya mwaka 2012.

Maoni ya wananchi:

Baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusu matukio hayo walionyesha wazi kusikitishwa, na kusema hata kama wafungwa ni wakosaji, lakini bado wana haki ya kuishi kama binadamu wengine.

Mzee Sylyvester Mosha, mwalimu mstaafu, alilaani vitendo hivyo na kuzitaka mamlaka husika kuchunguza utendaji kazi wa askari Magereza ndani ya magereza na mahusiano yao na wafungwa kwa ujumla.

“Hizi tetesi za wafungwa kupigwa na wakati mwingine kuuawa zimekuwapo kwa muda mrefu, lakini sidhani kama Serikali imeshafanyia kazi suala hili kwa dhati, sasa tukio la Kisongo liwe chachu kwa Serikali kuchukua hatua.

“Katika hali ya kawaida, magereza ndio watuhumiwa, halafu iweje magereza hao hao wajichunguze? Huu ni mchezo na kupoteza fedha za walipa kodi. Kwa nini isiundwe tume huru ikachunguza, na kama ikibaini ukweli, basi watuhumiwa wafikishwe mahakamani,” alisema.

Mkazi mwingine wa Kijenge mjini Arusha ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kitendo cha Jeshi la Magereza kuunda timu kuchunguza kinathibitisha kuwapo kwa tukio lisilo la kawaida.

Alisema; “Wafungwa ni binadamu kama binadamu wengine, kwa hiyo nao wanakufa, lakini hatua ya kutuma ujumbe kuchunguza tukio hilo, ni dhahiri kifo hicho kina utata, hivyo haikuwa sahihi magereza kujichunguza wenyewe, watu wengine wakawachunguze.

“Hata wafungwa wanaopigwa na kuvunjwa miguu au kupasuliwa vichwani na marungu, nao inabidi tuhoji hizo mamlaka magerezani, kwani kumuadhibu mfungwa ni mpaka umvunje mguu au umpasue kichwa hadi akashonwe? Huu unyama ukomeshwe mara moja.”

CHANZO: RAI
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment