Dr Shen aanza ziara rasmi mkoa wa kaskazini Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein leo anatarajiwa kuanza ziara katika Mkoa wa Kaskazini Unguja baada ya hapo jana kumaliza ziara yake ya siku mbili katika Mkoa wa Kusini Unguja.

 Akifanya majumuisho ya ziara yake katika Mkoa wa Kusini Unguja Rais Shein aliwataka Viongozi wa Serikali ya Mkoa huo kumaliza matatizo yanayoukabili Mkoa huo ikiwemo tatizo la Utoro Shuleni sambamba na kumaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu katika Mkoa huo.

 Alisema Suala la utoro katika Mkoa huo limeshamiri sana ambapo wastani wake katika Skuli za Mkoa huo ni Asilimia sita kwa wanafunzi wa Skuli za Msingi na Asilimia saba kwa Sekondari ambao wamekuwa wakitoroka Skuli.

 “Nitakapofanya Ziara nyingine katika kipindi kingine cha miezi sita inayokuja katika mkoa huu nataka taarifa yenu ya Mkoa ieleze kuwa Suala la Utoro limeisha” alisisitiza Dkt. Shein. Aidha kwa upande wa Migogoro ya Ardhi Dkt Shein aliwataka Viongozi wa Mkoa huo kufanya kazi kwa mashirikiano kuhakikisha kuwa migogoro ya Ardhi inamalizwa katika Mkoa huo.

 Dkt Shein aliwataka pia Viongozi wa Mkoa huo kuwatumikia Wananchi kwa karibu sana ili Wananchi hao waendelee kuwa na Imani na viongozi wao.

 Kuhusu Nyumba zilizojengwa na Serikali kwa Makaazi ya Wananchi wa Mpapa na vitongoji vyake Rais Shein amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kuzikodisha kwa watu wasiohusika ili kutimiza lengo lililopangwa.

 “Nakwambie Nyumba za Mpapa si nyumba za Watu wa Mjini inashangaza kuona Mtu wa Mjini kakodishwa nyumba hizo wakati Wahusika wa Mpapa wapo” alionya Dkt. Shein. Aidha Dkt Shein amepongeza maendeleo ya kilimo katika Mkoa huo na kuahidi Wananchi kuwa Serikali itaendelea kuwahudumia Wakulima ili kuinua Sekta hiyo muhimu.

 Amesema Jitihada zinaendelea kufanywa kuhakikisha kuwa pembejeo za kilimo zinapatikana vya kutosha huku akiwataka Wakulima kutumia ushauri wa Mabwana Shamba katika shughuli zao za kilimo.

 Dkt Shein alipata fursa ya kukagua Miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Mashamba ya Kilimo cha Mpunga, Maji safi na Salama, Skuli ambapo kwa ujumla alipongeza maendeleo yaliyofikiwa na Mkoa wa Kusini. Katika ziara yake ya siku tatu inayoanza leo Mkoa wa Kaskazini Unguja Dkt. Shein pia anatarajiwa kukagua Miradi mbalimbali ya maendeleo na kupata taarifa zake ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kutembelea Mikoa yote ya Unguja na Pemba kila ifikapo kipindi cha miezi sita.

 IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR, 12/03/2013
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment