Baadhi ya matukio hulenga kubadilisha mijadala ya jamii


NA HILAL K. SUED



TULIKUWA tumefikia wapi vile? Yaani kabla ya hili la kupigwa vibaya kwa Absalom Kibanda na lile lililofuata la video ya Wilfred Lwakatare? Nawaomba tusisahau. Tulikuwa katikati ya sakata la kufeli kwa wingi wa wanafunzi waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne, suala ambalo liliibua mjadala mkubwa na mzito katika jamii ulioiweka serikali mahala pagumu kweli kweli. 

Pamoja na jitihada kubwa za viongozi wa serikali na wanasiasa wa chama tawala, hoja ya msingi ilibakia pale pale, kwamba serikali ndiyo ya kubeba mzigo kwa kuzorota kwa viwango vya elimu nchini. 

Na si katika sekta ya elimu tu, bali kwa takriban kila sekta – kama vile afya, kilimo na usafiri. Kwa usafiri nina maana ya usafiri wa umma – hususan ule wa treni ambao wananchi wengi wa kipato cha chini hutegemea.

Lakini kabla ya Kibanda na Lwakatare kulikuwapo lile sakata la gesi ya Mtwara ambalo pia liliiweka serikali mahala pabaya – kwa kuonekana kutokuwa makini katika uvunaji wa maliasili na kuipeleka sehemu nyingine nchini bila ya kuangalia kwanza hali ya kimaendeleo ya eneo husika. Baadaye serikali ilionekana inasalimu amri. 

Wadadisi wa mambo wanasema masuala haya, kwa kuwa hayapatiwi ufumbuzi wa dhati ambao hakika ungekuwa wa kudumu, yana tabia ya kujirudia na kinachotakiwa kwa suala kurudi tena ni kwa jambo moja hasi kujitokeza na serikali kujikuta ina haha kutokana na kubanwa tena kwenye kona kwa sababu ya kutoonyesha umakini (clumsiness).

Kwa mfano – kwa vile suala la madaktari halikumalizwa kwa njia muafaka wa kuridhisha kwa pande zote husika, basi litarudi tu – na hasa kule kunakodaiwa “kumalizwa” kwake kuliambatana na tukio la kusikitisha – la kutekwa na kupigwa Dk. Steven Ulimboka, mwanaharakati aliyekuwa anatetea masilahi ya madaktari. 

Swali kubwa hapa la kujiuliza ni je, matukio haya ya kutekwa watu, kupigwa na kuumizwa na hata kuuawa (kama vile Mchungaji Evarist Mushi wa huko Zanzibar) hupangwa kimakusudi ili kuwaondoa wananchi kwenye mada ya masuala yanayoiweka serikali pabaya?

Na tunapotaja kuuawa kwa Mchungaji Mushi kuna baadhi ya Wazanzibari niliokutana nao wanaamini kabisa tukio hilo lilipangwa ili kuwabadilishia wananchi wa Zanzibar ile mada yao kuu kuhusu suala la Katiba, suala ambalo kwa hakika limekaa vibaya kwa serikali zote mbili (ya Zanzibar na ya Muungano) katika kuuokoa muungano kwani muelekeo wa Wazanzibari wengi ni kwamba mfumo wa Muungano uliopo sasa hivi ni lazima ubadilishwe kuwapa Wazanzibari ‘uhuru’ (autonomy) zaidi.

Wao Wazanzibari wanasema wanaharakati wanaopigania kuwepo “uhuru’ zaidi kwa Zanzibar wanabadilishiwa mada kutoka ile inayolenga harakati hizo na kuipeleka kwenye masuala ya udini na ugaidi.

Sote tumeona baadhi ya wanasiasa wa huko Zanzibar, akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Seif Shariff Hamad alipomjia juu Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emmanuel Nchimbi, kwa kauli yake ya haraka haraka kwamba mauaji ya Mchungaji Mushi ulikuwa ni ugaidi. 

Wanahoji kwa vipi mauaji haya yawe ugaidi, wakati ya aina hiyo hiyo yakitokea Tanzania Bara hakuna anayekimbila haraka haraka kusema kwamba ni ugaidi?

Wazanzibari wengine wanahoji – inakuwaje “wauaji” wa RPC Barlow aliyeuawa Mwanza usiku wa manane walikamatwa na kupandishwa kizimbani siku chache tu baadaye, wakati “wauaji” wa Mchungaji Mushi aliyeuawa mchana kweupe hawajapatikana na kupandishwa kizimbani hadi sasa?

Kuna baadhi ya wachunguzi wa mambo wanasema kwa ujumla watawala – hasa katika nchi ambazo ufisadi katika ngazi za juu serikalini umeshamiri na serikali yenyewe kuonekana kupiga danadana katika kuishughulikia, huwa hawapendi kuona hali ya nchi ikiwa shwari mno, kwani ushwari huo hutoa mwanya kwa wananachi kuidadisi serikali kuhusu ufisadi huo, ambao huzorotesha utoaji wa huduma kwa jamii. 

Hivyo mara kwa mara hutafuta au kuanzisha kitu, tukio au jambo litakalowaondoa wananchi kuendelea kufanya udadisi huo, angalau kwa muda, hadi litakapopatikana jambo jingine la kuvuruga.

Mtindo huu wa kuwaondoa wananchi kwenye mijadala ya msingi dhidi ya watawala na ambayo ni hasi kwa utawala haukuanza majuzi tu, ulikuwapo hata wakati wa Utawala wa awamu ya Kwanza wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, ingawa si kwa namna ya hivi sasa.

Wanaokumbuka mwanzoni mwa miaka ya 80 kulikuwapo manung’uniko makubwa sana miongoni mwa wananchi kuhusu ukosefu wa bidhaa muhimu, na hivyo ghafla utawala ulianzisha ile vita dhidi ya wale waliyoitwa “wahujumu uchumi.” 

Cha kushangaza katika hili kilikuwa ni kwamba watuhumiwa walianza kutiwa mbaroni kabla hata ile sheria ya kuhujumu uchumi iliyojumuisha jinai ya kuhodhi bidhaa haijatungwa na Bunge.

Sheria ilikuja kutungwa baadaye ambayo ilisimika mfumo pekee wa kimahakama kuwashughulikia watuhumiwa, mfumo ambao uliunda mahakama maalum nje ya zile zilizoainishwa katika Katiba. 

Lawama nyingi, pamoja za kutoka nje ya nchi zilielekezwa kwa serikali kuhusu “ukiukwaji” huu wa Katiba hadi mwishowe mahakama hizo maalum zilizoundwa ziliondolewa na sheria yenyewe ya kuhujumu uchumi kufanyiwa marekebisho makubwa.

Na katika awamu hiyo ya kwanza, kulikuwapo mtindo wa kubadilisha noti katika muda wa kipindi kifupi sana na wengi waliona lengo hasa ni kuwatia kidogo msukosuko wananchi angalau kwa muda. Mara ya mwisho hii ilifanyika mwaka 1985 – kipindi kile kile cha hali ngumu ya maisha kutokana na ukosefu wa bidhaa muhimu. 

Hata hivyo sababu rasmi iliyotolewa kufanya hivyo ni kuwabana wale waliokuwa na fedha nyingi zilizofikiriwa kuwa haramu ziondoke katika mzunguko katika kile kilichoitwa kudhibiti mfumuko wa bei. Sababu dhaifu kweli kweli.

CHANZO: RAI
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment