MAREKANI NA CUBA ZAKUBALI ‘YAISHE’

Rais Barack Obama wa Marekani



Katika kile kinachoonekana kama mabadiliko makubwa ya kisera, Rais wa Marekani Barack Obama ametangaza kuwa nchi yake na Cuba zitarejesha uhusiano wa kideplomasia baada ya kuvunjika kwa zaidi ya miaka 50.

Akizungumza kutokea White House jana, Rais Obama alitangaza kuhitimishwa kwa kile alichokiri kuwa ni sera “ngumu” ya kuitenga Cuba ambayo haikuzaa matunda.

Rais Obama amesema kuwa ukurasa mpya umefunguliwa katika uhusiano wa nchi hizo mbili na kwamba anataka kuwa na majadiliano ya dhati na bunge la Congress kuhusu matarajio ya kuiondolea Cuba vikwazo vya kibiashara vilivyodumu kwa kipindi cha nusu karne.

"Siamini kama tunaweza kuendelea kufanya mambo yaleyale kwa zaidi ya miongo mitano halafu tukatarajia kupata matokeo tofauti. Vikwazo havijasaidia”, alisema Rais Obama akizungumzia vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Cuba.

Aidha, Rais huyo wa Marekani alitangaza kuwa nchi yake itafungua ubalozi mjini Havana, Cuba na kuongeza kiasi cha fedha ambacho kinaweza kutumwa kutoka Marekani kwenda Cuba.

Alisema kuwa Washington itawezesha na kuidhinisha miamala kati ya nchi hizo mbili, na kwamba upelekaji wa bidhaa kwenda Cuba utarahisishwa zaidi kwa wafanyabiashara wa Kimarekani.


Tangazo hilo linakuja katika wakati ambako kumekuwa na hali mpya ya hatua za kujenga uaminifu kati ya maadui hao wa muda mrefu, ikiwa ni pamoja na kuachiliwa huru kwa mfungwa wa Kimarekani Alan Gross na kachero mwingine, na pia kuachiliwa huru kwa Wacuba watatu waliofungwa Marekani.


Cuba na Marekani hazikuwa na uhusiano wa kidiplomasia tangu mwaka 1961. Waligeuka kuwa maadui wakubwa muda mfupi baada ya mapinduzi ya mwaka 1959 yaliyomuingiza madarakani Fidel Castro.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment