BOKO HARAM YAUA 33 NA KUTEKA 185 NIGERIA


The file photo shows Boko Haram Takfiri militants in Nigeria.
Wanamgambo wa Boko Haram


Kundi la Boko Haram la nchini Nigeria linadaiwa kuwateka watu 185 katika kijiji cha Gumsuri kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini humo leo, kundi hilo lilifanya shambulizi katika kijiji hicho lililowaua watu wasiopungua 33 na kuwateka wengine 185.

Shambulizi hilo linadaiwa kutokea Desemba 14; hata hivyo habari za tukio hilo zimetolewa leo baada ya manusura wa shambulizi hilo baya kufanikiwa kufika katika mji wa Maiduguri.

Maofisa katika eneo hilo wanasema kuwa mateka walibebwa kwenye magari ya wazi na kupelekwa katika msitu wa Sambisa, ngome ya kundi hilo.

Wakati huo huo, duru za kijeshi kutoka nchini Cameroon, jirani na eneo la mashariki mwa Nigeria, zinasema kuwa wanamgambo 116 wa kundi hilo wameuawa wakati wa mapambano na jeshi la Cameroon.

Mnamo Aprili 14, kundi la Boko Haram liliwateka wanafunzi wa kike 276 kutoka shule moja ya sekondari katika mji wa Chibok kaskazini mwa nchi hiyo.

Tukio hilo liliibua kelele kutoka kila kona ya dunia. Utawala wa Nigeria umekuwa ukikosolewa vikali kwa kushindwa kuzima ghasia zinazolikumba taifa hilo.

Kundi la Boko Haram – ambayo ina maana ya “elimu ya Kimagharibi ni haramu” – linasema kuwa lengo lake ni kuiondosha madarakani serikali ya Nigeria.
Kundi hilo limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo tangu lilipoanzisha uasi wake mwaka 2009. Mpaka sasa zaidi ya watu 10,000 wameshapoteza maisha katika mashambulizi hayo.


Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumiwa wakimbizi, Wanigeria wapatao 650,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya kundi hilo na wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani, huku maelfu ya watu wakikimbilia katika mataifa jirani.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment