Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Afghanistan, Ahmad Yousuf Nuristani (katikati), akizungumza na waandishi wa habari mjini Kabul, Afghanistan, leo Aprili 14, 2014.
|
Wagombea 6 kati ya 8 wanaowania kiti cha urais wa
Afghanistan wameyakataa matokeo ya awali yanayoonesha kuwa waziri wa zamani wa
mambo ya nje wa nchi hiyo, Dkt Abdullah Abdullah, anaongoza.
Tume Huru ya UChaguzi ya nchi hiyo (IEC) imetangaza kuwa
katika asilimia 10 za kura zilizohesabiwa, Dkt Abdullah alikuwa akiongoza kwa asilimia
41.9; Dkt Ashraf Ghani akiwa na asilimia 37.6 katika nafasi ya pili na Zalmai
Rassoul akiwa na asilimia 9.8 katika nafasi ya tatu.
Tume hiyo imesema kuwa mgombea anayeongoza anaweza
kubadilika kadiri kura zinavyoendelea kuhesabiwa.
Kufuatia tangazo hilo, wagombea hao waliyakataa matokeo
na kutaka ufanyike uchunguzi wa tuhuma za wizi wa kura.
Tuhuma za wizi wa kura zinaonekana kushika kasi, lakini
tume inayohusika na malalamiko ya uchaguzi imesema kuwa itachukua wiki kadhaa kabla
ya kulimaliza suala hilo.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuwepo utulivu
mpaka zoezi la kuhesabu kura litakapokamilika. Zoezi hilo litaendelea mpaka
Aprili 20 huku matokeo yakitarajiwa kutangazwa Aprili 24.
Iwapo hatopatikana mgombea atakayepata zaidi ya asilimia
50 ya kura, basi uchaguzi wa marudio utafanyika mwishoni mwa mwezi Mei.
Uchaguzi huo unafanyika katika wakati ambapo vikosi vya
kimataifa vinapanga kuondoka nchini humo mwishoni mwa mwaka huu.
Licha ya uwepo wa maelfu ya vikosi hivyo kwa zaidi ya miaka
12, ghasia zimeendelea kuiandama nchi hiyo na ukosefu wa amani unaendelea kuwa
changamoto kuu.
0 comments:
Post a Comment