WATU 13 WAUAWA KATIKA GHASIA ZA MAGENGE YA ‘UNGA’ NCHINI MEXICO

Medical personnel remove the body of a victim killed in drug violence in Monterrey, Mexico. (File photo) 


Na Kabuga Kanyegeri

WATU kumi na tatu wamepoteza maisha katika ghasia zinazohusiana na madawa ya kulevya katika mji wa kaskazini mashariki wa Matamoros nchini Mexico.

Matukio matatu tofauti ya kushambuliana yametokea leo Jumapili katika mji huo wa kaskazini mwa jimbo la Tamaulipas.

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya jimbo, matukio mawili yalitokea baina ya majambazi na vikosi vya usalama vya Mexico. Watu 8 wamepoteza maisha katika mapambano hayo.

Aidha, wanaume wanne na mwanamke mmoja walipigwa risasi na kufa hapo hapo katika mapambano yaliyotokea mapema leo baina ya makundi ambayo hayakutambuliwa.

Jimbo la Tamaulipas limepata umaarufu wa kuwa miongoni mwa majimbo yenye ghasia na uhalifu wa kutisha nchini Mexico.

Katika miaka ya hivi karibuni, magenge ya madawa ya kulevya yanayofanya biashara hiyo katika jimbo hilo yamefanya matukio kadhaa ya mauaji, mapambano ya silaha na utekaji wakati yakiwania udhibiti wa njia ya biashara hiyo kuelekea Marekani.

Hii ni changamoto nyingine kwa Rais Enrique Nieto, aliyeingia madarakani mwezi Desemba mwaka jana, ambapo aliahidi kukomesha ghasia za magenge hayo ambazo zimegharimu maisha ya watu wapatao 80,000 tangu mwanzoni mwa mwaka 2007.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa tangu Nieto aingie madarakani, kila mwezi watu 1,000 hupoteza maisha katika matukio yanayohusisha biashara ya madawa ya kulevya na jeshi la Mexico linaendelea kupambana na magenge hayo katika maeneo mengi ya nchi hiyo.


Mapema mwaka huu, Nieto alikiri kuwa mtandao wa magenge ya kihalifu una nguvu kubwa na yana udhibiti katika maeneo kadhaa ya nchi, ikiwa ni pamoja na majimbo ya  Michoacan, Mexico na Guerrero, licha ya kuongezwa kwa idadi ya wanajeshi katika maeneo hayo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment