KESI YA MURSI YAAKHIRISHWA MPAKA JANUARI 8

 

Na Kabuga Kanyegeri

MAHAKAMA nchini Misri imeakhirisha kesi inayomkabili rais wa kwanza kuchaguliwa kidemkrasia nchini humo, Muhammad Mursi, huku wafuasi wake wakiandamana nje ya mahakama.

Ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana hadharani baada ya kupinduliwa na jeshi miezi minne iliyopita, Mursi alifikishwa leo kwenye mahakama hiyo iliyoko katika chuo cha mafunzo ya polisi.

Kesi ya msingi ilisimamishwa mara tu baada ya kuanza. Kesi dhidi ya Mursi na washitakiwa wenzake imepangwa kuendelea Januari 8.

Uamuzi huo ulikuja baada ya washitakiwa kuanza kupaza sauti za kulipinga jeshi, wakisema kuwa hawayatambui mamlaka ya mahakama.

Mursi anaripotiwa kusema kuwa yeye ndiye rais halali wa Misri na kuitaka mahakama iache mara moja kile alichokiita kuwa ni idhilali kwa rais halali.

"Mimi ni Dk Muhammad Mursi, rais wa jamhuri… Hii mahakama ni batili,” Mursi alisema wakati kesi ikianza na kuongeza, “Haya yalikuwa mapinduzi ya kijeshi. Viongozi wa mapinduzi haya wanatakiwa kushitakiwa. Mapinduzi ni uhaini na ni jinai.”

Mursi, na wanachama 14 wa Vuguvugu la Udugu wa Kiislamu wanatuhumiwa kuchochea ghasia zilizosababisha kuuawa kwa watu 10. Vuguvugu hilo limeyaita mashitaka hayo kuwa ya kutengenezwa.

Kwa sasa usalama umeimarishwa nchini Misri huku kiasi cha polisi 20,000 wakitumika kudumisha usalama katika mitaa mbalimbali.

Wafuasi wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu wameandamana katika miji kadhaa na nje ya mahakama. Ripoti zinasema kuwa mamia ya waandamanaji wamekamatwa.

Mapema Ijumaa, maelfu ya watu waliingia mitaani nchi nzima kupinga mashitaka dhidi ya Mursi na kutaka kiongozi huyo arejeshwe madarakani.

Aidha, walitaka haki itendeke kwa wafuasi wenzao waliouawa katika operesheni ya jeshi dhidi yao baada ya kuondolewa kwa Mursi.

Idadi kubwa ya maafisa na wafuasi wa chama hicho wameshikiliwa na jeshi na vikosi vya polisi tangu miezi kadhaa sasa, huku mamia ya wafuasi wengine wakiuawa katika operesheni ya vikosi vya usalama dhidi yao.


Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment